Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR limerejea wito wake wa kupiga marufuku kulazimishwa wasaka hifadhi kurudi makwao nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC, ikiwa ni pamoja na wasaka hifadhi ambao madai yao yamekataliwa, katika majimbo ya Kivu Kaskazini, Kivu Kusini na Ituri.
Katika mkutano wake na waaandishi wa Habari jijini Geneva Uswisi hii leo Mkurugenzi wa Ulinzi wa kimataifa wa UNHCR Elizabeth Tan amesema wanatoa wito kwa serikali kuwashughulikia watu hao kama wakimbizi na waruhusiwe kuingia maeneo wanayoomba hifadhi kwa mujibu wa Mkataba wa OAU wa mwaka 1969 unaosimamia Masuala Maalumu ya Matatizo ya Wakimbizi Barani Afrika.
Bi Tan amesema watu wengi wanaokimbia machafuko DRC kuna uwezekano mkubwa wamekidhi vigezo vya Mkataba wa mwaka 1951 wa hali ya ukimbizi.
Mataifa yana wajibu wa kisheria na kimaadili kuwaruhusu wale wanaokimbia migogoro inayoendelea kutafuta usalama, kupewa hifadhi kwa mujibu wa Mkataba wa OAU wa 1969, na kama inavyotumika, chini ya Mkataba wa Wakimbizi wa 1951, na kutowarudisha wakimbizi makwao kwa lazima.
UNHCR inasema ushauri wanaoutoa dhidi ya wasaka hifadhi kulazimishwa kurejea makwao katika majimbo ya Kivu Kaskazini, Kivu Kusini na Ituri nchini DRC utaendelea kutumika hadi pale hali itakapoimarika vya kutosha ili kuruhusu wakimbizi kurudi makwao kwa usalama na heshima.
UNHCR pia imeeleza wasiwasi wake kuhusu kuongezeka mashambulizi dhidi ya raia, ikiwa ni pamoja na wale wanaoishi katika kambi za wakimbizi wa ndani mashariki mwa DRC.
Tangu tarehe 20 Oktoba, watu 188,000 wamekimbia makazi mapya kutokana na mapigano kati ya kundi la waasi la M23 na Jeshi la Kongo. Hata kabla ya ongezeko la hivi karibuni la watu kuhama, takriban Wakongo milioni 5.6 walikuwa wakimbizi wa ndani.
Wengine milioni 1 wamepata hifadhi katika nchi 22 barani Afrika, na kuifanya hali hiyo kuwa moja ya majanga makubwa zaidi ya kibinadamu ulimwenguni.
Idadi kubwa ya watu milioni 4.9, wamekuwa wakimbizi wa ndani kwa sababu ya migogoro katika ameneo ya Kivu Kaskazini, Kivu Kusini na Ituri huku watu karibu 700,000 wakiyahama makazi yao kutokana na hali mbaya ya hewa.