UNICEF: Vita vya Saudia vimeua, kuwafanya vilema watoto 11,000 wa Yemen

Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) limesema watoto 11,000 wa Kiyemen ama wameuawa au kusababishiwa ulemavu wa daima wa viungo tangu yalipoanza mashambulizi ya muungano vamizi wa kijeshi huko Yemen chini ya uongozi wa Saudi Arabia mwezi Machi 2015.

Hayo yamesemwa leo Jumatatu na Catherine Russell, Mkurugenzi Mkuu wa UNICEF ambaye ameongeza kuwa, mbali na maelfu kupoteza maisha, mamia ya maelfu ya watoto wengine wa Yemen wapo katika hatari ya kuaga dunia, kutokana na baa la njaa na magonjwa mengine yanayoweza kuzuilika.

Amebainisha kuwa, watoto milioni 2.2 wa Yemen wanasumbuliwa na utapiamlo wa kiwango cha juu, ambapo robo yao wakiwa na umri wa chini ya miaka mitano.

Russell ameongeza kuwa, akthari ya watoto hao wa Kiyemen wanaosumbuliwa na utapiamlo wapo katika hatari ya kukumbwa na maradhi ya kipindupindu, surua na magonjwa mengine yanayoweza kuzuilika kwa chanjo.

Kwa mujibu wa Shirika hilo la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa, katika kipindi cha miezi saba iliyopita, watoto 15 wa Kiyemen wameaga dunia kwa maradhi ya surua.

UNICEF imesema watoto  wasiopungua 1,400 katika mikoa saba ya Yemen ukiwemo mkoa wa Aden kusini mwa nchi hiyo walishukiwa kupatwa na ugonjwa wa surua kati ya mwezi Januari na Julai mwaka huu.

Vita vya muungano wa vamizi wa Saudia vimeifanya Yemen kukumbwa na janga kubwa zaidi la kibinadamu kuwahi kushuhudiwa duniani, huku mamilioni ya wananchi wa nchi hiyo maskini ya Kiarabu wakiathiriwa na njaa na maradhi.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *