Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) limetangaza kuwa, watoto wapatao milioni 4 nchini Pakistan wangali wanaishi kwenye maji machafuko yaliyosimama.
Taarifa ya UNICEF imebainisha kuwa, zaidi ya miezi minne tangu kutangazwa kwa hali ya dharura, zaidi ya watoto milioni 4 bado wanaishi karibu au kwenye maji ya mafuriko yaliyosimama na hivyo kutishia uhai na ustawi wao.
Kwa upande wa lishe, zaidi ya watoto 800,000 wamechunguzwa utapiamlo ambapo kati yao hao, 60,000 wamebainika kuwa na unyafuzi ambao ni pale mtoto anakuwa ni mwembamba kupindukia ukilinganisha na urefu wake na hivyo kupatiwa lishe maalum.
Huduma hiyo ya lishe imefikia takribani watu milioni 1.5 kupitia huduma za afya ya msingi. Halikadhalika watoto milioni 4.5 wamepatiwa chanjo dhidi ya Polio katika wilaya 16 zilizokumbwa na mafuriko.
UNICEF na wadau pia wamepatia zaidi ya watu milioni 1 huduma za maji safi na salama, bila kusahau vikasha vya kujisafi kwa watu milioni moja.
Pakistan mwaka huu imeathiriwa na mvua kubwa za masika kuwahi kushuhudwa nchini humo ambazo zimeuwa watu zaidi ya 1,700 wakiwemo watoto 647 na kupelekea wengine milioni 33 kukosa makazi. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, nyumba milioni mbili na shule 2700 zimebomolewa kwa mafuriko katika maeneo mbalimbali ya Pakistan.
Jumla ya watu milioni 9 huko wanakabiliwa na umaskini huko Pakistan kutokana na kupoteza ajira, mifugo yao, mavuno ya kilimo, nyumba, kufungwa shule,kuenea magonjwa mbalimbali ya kuambukiza na pia kupanda kwa bei za vyakula kufuatia janga hilo la mafuriko.