UTATA MASHARIKI YA KATI: Tahadhari yatolewa kwa Tanzania mgogoro wa Marekani, Iran

Mzozo huo umetokana na mpango wa nchi ya Iran wa kuzalisha nyuklia ikisema ni kwa ajili ya umeme, huku Marekani ikidai kuwa nchi hiyo ina mpango wa siri wa kutengeneza silaha za nyuklia.

Kutokana na hofu hiyo, nchi za Marekani, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na China zilikubaliana kuiwekea vikwazo Iran iwapo itaendelea na mpango huo.Mwaka 2015 Iran ilikubali kuweka saini mkataba wa kimataifa wa nyuklia ili iruhusiwe tena kufanya biashara na mataifa mengine duniani.

Licha ya Iran kusitisha uzalishaji huo, iliyalalamikia mataifa ya Ulaya kwa kushindwa kutekeleza ahadi zao za kulinda uchumi wa Iran dhidi ya vikwazo vya Marekani.Katika hatua nyingine, Iran imekiri kui-dungua ndege ya Ukraine aina ya Boeing 737-800 muda mfupi baada ya kupaa katika Uwanja wa Ndege wa Tehran.

Ndege hiyo ilianguka muda mfupi baada ya kuruka wakati Iran ikirusha makombora dhidi ya kituo cha kijeshi cha Marekani nchini Iraq kulipiza kisasi kwa mauaji ya Soleimani.Awali Mamlaka ya Anga ya Iran ilikanu-sha madai kuwa ndege hiyo ilitunguliwa, huku shinikizo la kimataifa likiongezeka kuitaka Iran ifanye uchunguzi unaoam-inika baada ya nchi kadhaa za magharibi kusema ilitunguliwa.

Akizungumzia chanzo cha mzozo huo, Balozi Charles Sanga aliyewahi kufanya kazi kama msaidizi wa Mwalimu Julius Nyerere alisema kwanza ni wasiwasi wa Marekani kwa kutojua uwezo wa Iran kivita na mwendelezo wa uporaji wa rasilimali.

“Vita ni suala linalopaswa kuepukwa kwa gharama yoyote ile, hata kama kutakuwa na sababu inayolazimisha vita. Katika Mashariki ya Kati, tuchukulie Iraq sababu walizotoa Marekani katika vita ile hakukuwa na sababu yoyote ile zaidi ya kutaka rasilimali ya nchi ambazo kwa Mashariki ya Kati hakuna zaidi ya mafuta, kwa hiyo ilikuwa ni vita ya mafuta. Haiwezi kukubalika kwa namna yoyote,” alisema.

Huku akitaja athari kubwa ya mzozo huo kuwa ni kuathirika kwa biashara za kimataifa ikiwemo ya mafuta, Balozi Sanga alisema kwa sasa Tanzania haiwezi kupaza sauti kukemea kama ilivyokuwa wakati wa Mwalimu Nyerere kwa kuwa mazingira yamebadilika.

“Mwalimu wakati ule alikuwa na msimamo, wakati ule ulikuwa ni wakati wa kupinga udhalimu wa aina yoyote ile. Ukweli ni kwamba ‘circumstances (mazingira), kwa sasa nchi yetu si kwamba tuko mstari wa mbele sana kwamba tunawatetea wanyonge wanaokandamizwa. Tunajaribu kuangalia nchi yetu masilahi yake yanapatikana wapi,” alisema.

Alizitaka nchi za Marekani na Iran kutumia Umoja wa Mataifa kutatua mzozo huo. “Kuna Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kuna nchi tano waende wakalizungumze. Tunaona Trump anasema anataka mazungumzo, lakini je, ni kweli yanatoka moyoni?”

Hata hivyo, kwa upande wake Profesa wa Historia kutoka Zanzibar, Abdul Sherrif alisema kama ilivyokuwa kwa vita ya kwanza na ya pili ya dunia, Tanzania kama zilivyo nchi nyingine duniani itaathirika hata kama haishiriki vita hivyo.

“Vita vya kwanza vya dunia viliathiri Tanzania kwa sababu Wajerumani na Uingereza walikuwepo. Hata vita vya pili, havikuja kupiganiwa hapa lakini tuliathirika. Kwa hiyo tujue vita ile haitawagusa tu wale bali pia itatugusa sisi,” alisema Profesa Sherrif.

Profesa Sherrif ameilaumu Marekani kwa kile alichokiita uchokozi kwa kumuua kiongozi wa kijeshi wa Iran, Solemani huku pia akilitaja Taifa la Israel akisema linalindwa na nchi ya Marekani dhidi ya mataifa ya Kiarabu.

“Hatutaki kuingia katika vita kule, lakini hatupaswi kukaa kimya, kwa sababu maovu yatakuja kwetu. Ilitakiwa kutolewa tamko maana mpaka sasa Tanzania hatujatoa lolote. (Serikali) Iseme kwamba tunataka usalama usio na ukandamizaji,” alisema Profesa Sheriff.

Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia cha Kurasini Dar es Salaam, Innocent Shoo alisema mzozo huo utayachochea makundi ya kivita yaliyopo katika nchi za Syria, Jordan, Palestina na Israel kupambana na hivyo kuvuruga usalama wa dunia.

Alisema kwamba madhara yake yatakuwa kwa nchi zote yakihusisha kuvurugika kwa uchumi ikiwa ni pamoja na kuathirika kwa upatikanaji wa mafuta.

“Marekani ina vituo vya kijeshi katika nchi za Djibout na Kenya, vinaweza kushambuliwa na kuathiri wananchi wa nchi hizo. Makundi kama Hezibollah, Fatah na Hamas yanaweza kushambulia popote pale duniani kwenye masilahi ya Wamarekani na watakaoumia ni wananchi wa nchi husika,” alisema Shoo.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *