Ndege za kivita za utawala haramu wa Kizayuni wa Israel zimeshambulia kwa makombora zaidi ya kumi kituo cha wanamapambano wa Muqawama wa Palestina katikati ya Ukanda wa Gaza.
Televisheni ya Aljazeera ya Qatar imeripoti kuwa, alfajiri ya kuamkia leo ndege za kivita za utawala wa kizayuni zimeshambulia kambi ya al Maghaazi iliyoko katikati ya Ukanda wa Gaza.
Kwa mujibu wa ripoti ya chaneli hiyo ya televisheni umeme wa baadhi ya maeneo ya Gaza umekatika kutokana na mashambulio hayo.
Jeshi la utawala haramu wa Kizayuni limedai kuwa mashambulio hayo yanafanyika kutokana na makombora yaliyofyatuliwa Ukanda wa Gaza kuelekea ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (Israel).
Msemaji wa jeshi la utawala huo ghasibu amethibitisha kufanyika mashambulio hayo ya anga na akaongeza kuwa Ukanda wa Gaza umelengwa na mashambulio alfajiri ya kuamkia leo.
Aidha amedai kwamba ngome moja ya harakati ya Hamas imeshambuliwa kwa makombora hayo.
Jana usiku, duru za utawala wa Kizayuni zilitangaza kuwa ving’ora vya hali ya hatari vilisikika katika vitongoji vya Nairim, Kizovim na Ainu-Thaalithah kusini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Kwa mujibu wa duru hizo maroketi kadhaa yalifyatuliwa kutoka Gaza kuelekea ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na kupelekea kuwashwa mtambo wa Kuba la Chuma na ving’ora vya hali ya hatari.
Makombora kuelekea ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni yamefyatuliwa kufuatia hujuma na uvamizi uliofanywa na Wazayuni katika kambi ya Jenin, ambapo vijana wawili Wapalestina Farouq Jamil Hassan Salamah na Muhammad Ziyad Sabaanah waliuawa shahidi na wengine wanne walijeruhiwa.