Utawala wa Israel waogopa kuona bendera ya Palestina ikipeperushwa

Utawala wa Kizayuni umewakamata waandamanaji watatu waliokuwa wakipeperusha bendera za Palestina katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu ambazo zimepachikwa jina la Israel.

Kubebwa na kupeperushwa bendera ya Palestina na watu wa nchi mbali mbali duniani katika Kombe la Soka la Dunia la 2022 huko Qatar ni jambo ambalo limeibua hofu na wasi wasi mkubwa miongoni mwa maafisa wa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Kwa mujibu wa gazeti la Kizayuni la Yedioth Ahronoth, askari wa Israel waliwakamata watu wawili katika mji wa Haifa na mwingine katika kitongoji cha Barkan kwa kosa la kupeperusha bendera ya Palestina katika maandamano.

Askari hao wa utawala wa Israel walikuwa wamewataka waandamanaji hao waweke chini bendera za Palestina lakini walikataa na hivyo walikamatwa na kupelekwa kizuizini kwa ajili ya kusailiwa.

Kupeperushwa bendera za Palestina katika ardhi ambazo Israel inazikalia kwa mabavu kunawakasirisha sana watawala wa Tel Aviv. Mwezi Juni utawala wa Kizayuni wa Israel ulipitisha sheria na kusema, ‘kupeperusha bendera ya adui (Palestina) ni kinyume cha sheria.’

Katika Kombe la Dunia la Qatar, Timu ya Soka ya Morocco imepata umaarufu mkubwa baada ya kupeperusha bendera ya Palestina. Aidha mashabiki wa Morocco na wale wa nchi zingine hasa za Kiarabu wamekuwa wakipeperusha bendera za Palestina uwanjani kama njia ya kubainisha kufungamana kwao na harakati za kukomboa ardhi za Palestina zinazokoloniwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel.

Aidha mashambiki wengi wa soka nchini Qatar wamekataa kuhojiwa na vyombo vya habari vya utawala wa Israel. Katika tukio moja shabiki mmoja wa soka alimfahamisha mwandishi wa televisheni moja ya Israel kwamba, hakuna nchi inayojulikana kwa jina la Israel bali ni ardhi za Palestina zilizokabiliwa kwa mabavu na kupachikwa jina bandia la Israel.

 

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *