Utawala wa Kizayuni wa Israel watiwa kiwewe na droni za Iran

Chombo kimoja cha habari cha utawala wa Kizayuni kimeelezea kuingiwa na hfu kubwa kutokana na kuimarika teknolojia ya ndege zisizo na rubani (droni) za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika miaka ya hivi karibuni na kugeuka teknolojia hiyo kuwa sehemu muhimu katika mkakati wa kujihami taifa hili la Kiislamu.

Gazeti la Jerusalem Post limeandika hayo katika toleo lake la leo Jumanne na kuongeza kuwa, kujiimarisha Iran kwa ndege za kisasa zisizo na rubani zikiwemo zinazoshambulia kwa kujiripua aina ya Kamikaze, kumeongeza uwezo wa kijeshi wa Jamhuri ya Kiislamu katika pande tofauti na hilo ni tishio kwa usalama wa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Maendeleo ya droni za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran muda wote ni makubwa kiasi kwamba ndege zisizo na rubani za Iran hasa katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, zimeonesha uwezo wake mkubwa katika medani mbalimbali za mapambano, za uchunguzi, za kugundua maficho ya adui na za kushambulia. Vita vilivyotokea kwenye eneo la Asia Magharibi katika kipindi hicho, vimezipa uwanja droni za Iran kuonesha uwezo wake wa kipekee mbele ya walimwengu.

Ripoti ya gazeti la Kizayuni la Jerusalem Post imeongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inawapa waitifaki wake ndege zisizo na rubani na kuwaimarisha kijeshi waitifaki wake hao katika eneo hili suala ambalo ni hatari sana kwa Israel.

Wataalamu na makamanda wa kijeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wamekuwa wakikiri mara chungu nzima kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina uwezo mkubwa wa makombora na ndege zisizo na rubani.

Moja ya mkakati mkuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kuhakikisha adui hafikirii kabisa kulivamia kijeshi taifa hili.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *