Faraan : Waandamanaji wenye hasira nchini Bahrain wameteketeza kwa moto bendera za utawala wa Kizayuni wa Israel wakilaani safari ya siku mbili ya Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel, Naftali Bennet katika nchi hiyo ndogo ya Ghuba ya Uajemi.
Maandamano yamefanyika kote katika nchi hiyo huku waandamanaji wakikanyaga bendera za Israel na kuziteketeza huku wakiwa wamebeba mabango yaliyoandikwa, ‘Naftali ondoka.’
Maandamano hayo yamejiri huku kukiwa na sheria kali ambazo zimewekwa na maafisa wa usalama nchini humo kuzuia mijumuiko ya kulaani safari ya waziri mkuu wa Israel nchini humo.
Naftali Bennet Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni Jumanne alielekea nchini Bahrain kwa mwaliko rasmi wa Hamad bin Isa Aal Khalifa, mfalme wa nchi hiyo.
Jumuiya ya kitaifa na Kiislamu nchini Bahrain ya Al-Wifaq imeitaja safari ya Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel huko Manama mji mkuu wa Bahrain kuwa ni usaliti wa utawala wa Aal Khalifa kwa watu wa nchi hiyo na kusisitiza kuwa, safari hiyo inakiuka maadili na ni kitendo chenye lengo la kuyachochea mataifa ya Kiarabu na Kiislamu.
Sheikh Hossein al Daei Naibu Katibu Mkuu wa al Wifaq amepinga vikali ziara hiyo ya Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni mjini Manama na kusema, wananchi wa Bahrain wataendelea kutetea na kuunga mkono malengo ya Palestina na kwamba hawaafiki hatua yoyote ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala ghasibu wa Israel.