Uturuki yataka vikwazo dhidi ya Iran na Venezuela viondolewe ili kupunguza bei ya mafuta duniani

Uturuki imetoa wito wa kuondolewa vikwazo vya nchi za Magharibi dhidi ya Iran na Venezuela huku kukiwa na mzozo wa nishati duniani uliochochewa na oparesheni ya kijeshi ya Russia nchini Ukraine.

Ongezeko la bei ya nishati hasa petrol na gesi duniani ni chanzo cha kupanda gharama ya maisha kwa mamia ya mamilioni ya watu duniani kote..

Akizungumza Ijumaa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu amesema, “Ulimwengu mzima unahitaji mafuta na gesi asilia ya Venezuela… Kwa upande mwingine, kuna vikwazo kwa mafuta ya Iran.” Ameendelea kusema kuwa iwapo dunia inataka bei ya mafuta ya petrol na gesi ishuke basi vikwazo vinapaswa kuondolewa dhidi ya Iran na Venezuela.

Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Uturuki alisema matatizo ya dunia hayawezi kutatuliwa kwa kutoa vitisho dhidi ya nchi zingine.

Mnamo Agosti, Waziri wa Mafuta wa Iran Javad Owji alionya juu ya shida ya nishati ya ulimwengu msimu huu wa baridi, akisema Tehran iko tayari kuongeza mauzo yake ya mafuta kwa kiwango kikubwa ikiwa vikwazo vitaondolewa nchini.

Akizungumza siku moja baada ya mkutano wa Jumuiya ya Nchi Zinazouza Petroli Duniani na washirika wake, shirika linalojulikana kwa jina la OPEC+, Agosti 4, Owji alisisitiza matamshi ya awali ya Iran kwamba nchi hiyo itaweza kurejea mara moja katika mauzo ya mafuta karibu mapipa milioni 2.8 kwa siku.

Kama mmiliki mkubwa wa rasilimali (zilizounganishwa) za mafuta na gesi duniani, tuko tayari kuongeza uzalishaji wa mafuta ghafi hadi kiwango cha kabla ya vikwazo kwa muda mfupi iwezekanavyo,” Owji alisema.

Alieelezea matumaini yake kuwa serikali za Magharibi zitatumia mbinu ya kimantiki zaidi katika kushughulikia suala la mafuta huku akisisitiza kuwa kuongezeka kwa usambazaji wa mafuta na gesi kutoka Iran kutasaidia kurejesha uwiano na utulivu katika masoko ya kimataifa.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *