Katika taarifa rasmi, Kanisa la Vatican limeomba radhi kwa Russia kutokana na matamshi ya kibaguzi yaliyotolewa na kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis, dhidi ya Wachechnya na Waburyati.
Akizungumzia hatua ya Kanisa la Vatican ya kuomba radhi rasmi kutokana na kauli za kibaguzi za Papa Francis, kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani dhidi ya Wachechnya na Waburyati, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia, Maria Zakharova amesema hatua hiyo ina maana kwamba Vatican ina uwezo wa kufanya mazungumzo na kusikiliza pande zote.
Zakharova amesema: “Kwa mshangao mkubwa, ndani ya saa chache zilizopita, tumepokea barua kupitia njia za kidiplomasia za Vatican, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Vatican Pietro Parolin, ambayo ilikuwa na taarifa kuhusu matamshi ya awali ya Papa.”
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia ameongeza kuwa, taarifa hiyo inasema waziwazi kwamba, “Katibu Mkuu wa Vatican anaiomba radhi Russia na kwamba Vatican inawaheshimu sana watu wote wa Russia, utu, dini na utamaduni wao..”
Awali kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis aliwataja wale waliouawa nchini Ukraine kuwa ni “mashahidi” na kudai kwamba “watu makatili zaidi pengine ni kama Wachechnya na Waburyati ambao wana asili ya Kirusi lakini ni wageni kwa utamaduni wa Russia.”
Wakati huo, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia, Maria Zakharova aliitaja kauli hiyo ya Papa Francis kuwa haikubaliki na kusema, “Huu ni upotovu ambao hatuwezi hata kupata jina lake!”