Idadi ya vifo imeongezeka na kufikia watu 16 huku watu wengine 19 wakiwa bado hawajulikani walipo baada ya dhoruba kali ya kimbunga cha tropiki iliyopewa jina la Cheneso kuipiga Madagascar. Hayo ni kwa mujibu wa taarifa ya jana Alkhamisi iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Kudhibiti Hatari na Majanga ya nchi hiyo, (BNGRC).
Taarifa ya ofisi hiyo ya BNGRC imeongeza kuwa, watu 55,421 wameathiriwa na kimbunga hicho katika mikoa 15; kati yao, watu 25,678 wamehamishwa. Taarifa hiyo pia imesema, maji yamefurika kwenye nyumba 13,356 huku nyumba nyingine 500 zikiharibiwa kabisa.
Kimbunga cha Cheneso kilitua Januari 19 kwenye pwani ya kaskazini mashariki mwa nchi ya kisiwa cha Bahari ya Hindi na kuelekea kusini-magharibi.
Kufikia Alkhamisi alasiri, Cheneso ilikuwa iko kilomita 175 magharibi mwa pwani ya magharibi ya Madagascar. Kimbunga hicho kilikuwa kinasonga polepole kuelekea kusini-magharibi kwa kasi ya kilomita 7 kwa saa na kinatarajiwa kusonga kwa zaidi ya kilomita 130 kutoka maeneo ya pwani katika siku mbili zijazo.
“Mvua kubwa bado inatarajiwa kunyesha katika pwani ya magharibi mwa nchi,” imeonya taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa ya Madagascar.
Wilaya kadhaa katika mkoa wa Mahajanga za kaskazini magharibi mwa Madagascar ndizo zilizoathiriwa zaidi kutokana na mafuriko pamoja na barabara zinazoziunganisha wilaya hizo kuelekea mji mkuu, Antananarivo.
Mbali na mafuriko hayo, Ofisi ya Taifa ya Kushughulikia Maafa na Majanga ya Kimaumbile ya Madagascar imesajili matukio kadhaa ya maporomo ya udongo.
Olga Rasoanirina Mkurugenzi wa mkoa wa Boeny ameeleza kuwa, wamewapa makazi ya muda watu kadhaa walioathiriwa na kimbunga cha Cheneso tangu Jumapili iliyopita. Amesema wameandaa maeneo katika shule moja ya serikali ambapo waathirika wa mafuriko wanapatiwa huduma ikiwemo chakula.