Mashambulizi ya Jeshi la Somalia (SNA) dhidi ya kundi la magaidi wa Al-Shabaab yamepata mafanikio mapya baada ya vikosi vyake kuukomboa mji wa Runirgoud, ngome ya mwisho ya magaidi hao wakufurishaji huko Shabelle ya Kati, takriban kilomita 240 kaskazini mashariki mwa mji mkuu Mogadishu.
Kulingana na Jenerali Abdullahi Ali Anod, msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Somalia, kikosi cha Jeshi la Kitaifa la Somalia kinachoungwa mkono na walinzi wa eneo hilo kiliukomboa mji wa Runirgoud kutoka kwa Al-Shabaab siku ya Ijumaa.
Akihutubia vyombo vya habari, Jenerali Anod alisema kwamba vikosi vinavyounga mkono serikali kwanza vilijipenyeza kwenye vijiji vilivyo karibu na mji wa Runirgoud na kuwakabili wanamgambo wa Al-Shabaab katika mapigano makali siku ya Alhamisi.
“Hatimaye, wanajeshi wa SNA, pamoja na wanamgambo wanaounga mkono serikali, waliuteka mji huo mapema Ijumaa,” Anod alisema.
Wiki mbili zilizopita, Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud alisema kwamba oparesheni za kukomboa Shabelle ya Kati, mojawapo ya mikoa miwili iliyounda Jimbo la Hirshabelle katika Somalia ya Kati, zilikuwa karibu kukamilika.
“Ni Runirgoud pekee iliyosalia kukombolewa katika Shabelle ya Kati,” alisema Rais Mohamud.
Mafanikio hayo yamepetikana kutokana na kuhusishwa na wanamgambo wanaounga mkono serikali ambao ni sehemu ya juhudi zinazoendelea za kukomboa maeneo yanayodhibitiwa na magaidi wa Al-Shabaab. Wamamgambo hao ambao ni maarufu kama Mo’awisley aghalabu ni wa jamii za wafugaji na wamefanikiwa kuwatimua kwa urahisi magaidi wa Al Shabab.