Rais Ibrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran adhuhuri ya jana Jumatatu aliwasili mjini New York akiuongoza ujumbe wa ngazi za juu wa Tehran kwa minajili ya kushiriki katika mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Akizungumza na waandishi wa habari alibainisha ratiba ya safari yake mjini New York. Rais wa Iran sambamba na kubainisha kwamba, Umoja wa Mataifa haupaswi kuwa ni taasisi ya madola makubwa amesisitiza kuwa: Vikwazo, ugaidi, vita na umwagaji damu ni matokeo ya uchukuaji maamuzi ya upande mmoja. Suala la uchukuaji maamuzi ya upande mmoja ambapo katika zama za leo Marekani ndio dhihirisho lake, daima limekuwa likikosolewa na mataifa pinzani na yanayokosoa siasa na hatua za Marekani.
Katika fremu ya sera hizo za upande mmoja na katika kipindi cha miongo miwili ya hivi karibuni, Marekani imeanzisha vita kadhaa katika eneo la Asia Magharibi kama Iraq na Afghanistan na vilevile imekuwa na uingiliaji mambo huko Syria kwa maslahi ya makundi ya kigaidi lengo likiwa ni kuiondoa madarakani serikali halali ya Damascus na wakati huo huo kuandaa uwanja wa kuzusha machafuko na ukosefu wa usalama katika eneo hili sambamba na kueneza ugaidi.
Vita vilivyoanzishwa na serikali vamizi ya Marekani vimesababisha kuuawa mamia ya maelfu ya watu Asia Magharibi na wakati huo huo, himaya na uungaji mkono wa Washington kwa ugaidi hususan kwa makundi ya kigaidi na kitakfiri kama Daesh umepelekea kutokea jinai ambazo hazijawahi kushuhudiwa katika mataifa ya Syria na Iraq na hatua iliyofuata huko nchini Afghanistan. Kama alivyosema Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kuwa, ugaidi na uungaji mkono unaotolewa kwa makundi ya kigaidi, hii leo umepelekea kutokea wimbi kubwa la wakimbizi duniani.
Marekani hasa katika kipindi cha urais wa Donald Trump ilichukua mkondo mpana zaidi wa kuchukua maamuzi ya upande mmoja, yasiyo ya kisheria na ya kidhalimu dhidi ya mataifa mengine ya dunia hususan zile nchi zinazojitawala na zisizokubali kuburuzwa. Sera hizo za Marekani hazikupelekea kutokea tu makabiliano ya kisiasa na kibiashara baina yake na washindani wake kama China na kadhalika, bali ziliibua mzozo baina ya Washington na washirika wake wa Ulaya.
Nukta muhimu hapa ni hii kwamba, Marekani katika kipindi cha utawala wa Rais Joe Biden pia siyo tu kwamba, haijaacha utendaji huu wa uchukuaji maamuzi ya upande mmoja, bali imekuwa iking’ang’ania kuendeleza sera hizo. Mfano wa wazi wa hilo ni sisitizo la Washington la kuwa kinara wa kambi ya Magharibi katika hatua zinazochukuliwa dhidi ya Russia kwa kisingizio cha vita vya Ukraine.
Suala ambalo limekuwa mjadala mkubwa kuhusiana na uchukuaji maamuzi wa upande mmoja wa Marekani ni vikwazo vyake vya upande mmoja, visivyo vya kisheria na vya kidhalimu dhidi ya nchi nyingine. Filihali Marekani inahesabiwa kuwa nchi inayoongoza duniani kwa kuyawekea vikwazo mataifa mengine.
Licha ya kuwa, Marekani ikifanya hivyo kwa visingizio mbalimbali kama vya kisiasa, kibiashara, kiusalama na hata masuala ya haki za binadamu hususan mataifa ambayo ni washindani wake, lakini hiyo ni sababu ya kidhahiri tu, kwani ukweli wa mambo ni kuwa, Washington hufanya hivyo ikifuatilia malengo yake binafsi.
Kuhusiana na hilo, Rais Ibrahim Raisi anasema: Vikwazo vinatumiwa na madola makubwa kama wenzo wa kuyashinikizia mataifa mengine na mkabala na hilo mataifa hayo nayo yatachukua hatua kama hizo jambo ambalo linakinzana na amani, utulivu na usalama wa dunia na wanaodhurika ni walimwengu.
Umoja wa Mataifa nao mara kadhaa umekosoa vikwazo vya upande mmoja vya Marekani hususan katika kipindi cha msambao wa maradhi ya Covid-19 ambapo uliitoa mwito wa kuondolewa au kupunguzwa vikwazo hivyo ili kuzirahishia nchi zilizowekewa vikwazo kuweza kupata dawa na vifaa vya tiba.
Inaonekana kuwa, kutokana na athari haribifu za vikwazo vya upande mmoja vya Marekani kuna udharura wa kuweko mshikamano baina ya mataifa yaliyowekewa vikwazo kama kuanzishwa muungano wa kimataifa dhidi ya vikwazo ili kuifanya Washington ilazimike kutazama upya suala hilo hasa kutokana na kuweko mashinikizo ya pamoja ya kimataifa dhidi yake.