Vikwazo vinavyoendelea kuwekwa na magaidi wa kundi la al-Shabaab katika baadhi ya maeneo ya Somalia vinazidisha hali mbaya ya kibinadamu katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Bakool kusini magharibi mwa Somalia ni mojawapo ya mikoa iliyoathiriwa zaidi na ukame. Eneo hilo limekuwa chini ya vizuizi vya al-Shabaab kwa zaidi ya muongo mmoja, huku njia pekee ya kuwafikia watu wanaohitaji msaada wa kibinadamu ikiwa ni kwa ndege au kutumia mikokoteni ya punda kusafirisha chakula.
Omar Atu, meya wa mji mkuu wa jimbo la Bakool Hudur, ameliambia Shirika la Anadolu kwamba magaidi wa al-Shabaab wiki iliyopita waliteketeza zaidi ya mikokoteni minne ya punda iliyobeba chakula kilichohitajika sana katika eneo hilo.
Eneo jirani la Gedo pia limeathiriwa na vizuizi vya al-Shabaab na vikwazo vya kibinadamu. Ali Yussuf Abdullahi, msemaji wa utawala wa eneo la Gedo, ameliambia Shirika la Anadolu kwamba ingawa hali huko ni tofauti, wameona magaidi wa al-Shabaab wakizuia shughuli za kibinadamu.
Magaidi hao pia wamewaua wahandisi kadhaa waliokuwa wakichimba kisima cha maji mkoani humo, amesema. Amesema lengo kuu la kundi la kigaidi ni kushinikiza wakazi wa eneo hilo kuacha kuunga mkono serikali.
Eneo la Hiran, ambalo limekumbwa na machafuko baada ya magaidi wa al-Shabaab kuharibu visima vya maji na kuchoma magari yaliyokuwa yamebeba chakula, pia limeathirika, ingawa serikali imesema imekomboa sehemu kubwa ya eneo hilo kutoka kwa kundi hilo.
Mkuu wa Wilaya ya Mahas Mumin Mohamed Halane ameliambia Shirika la Anadolu kwamba Wasomali wamechoshwa na mbinu za vikwazo na tamaa ya kundi la kigaidi la al-Shabaab.
Misimu minne ya mvua ya chini ya wastani nchini Somalia imezuia usambazaji wa chakula kinachokuzwa nchini humo katika masoko kote nchini.
Kulingana na Umoja wa Mataifa, makadirio yanaonyesha kuwa msimu wa mvua Aprili-Juni na mavuno ya msimu wa Septemba-Oktoba yote yalikuwa 50% chini ya wastani wa muda mrefu. Kupanda kwa bei ya vyakula katika soko la kimataifa pia kumesababisha hali kuwa mbaya zaidi nchini Somalia.
Hivi sasa, kuna zaidi ya watu milioni 6.7 wanaokabiliwa na njaa nchini, amesema Ishaku Mshelia, naibu mratibu wa dharura wa Ofisi ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) nchini Somalia. Somalia ilitangaza ukame wa sasa kuwa “dharura ya kitaifa ya kibinadamu” mwishoni mwa 2021. Umoja wa Mataifa pia ulitoa tahadhari hiyo na kusema kuwa kuna uwezekano njaa ikatokea katika baadhi ya maeneo ya Somalia huku ukame ukiendelea kuwa mbaya zaidi.