Viongozi wa dini: Toeni ushirikiano mhesabiwe, Sensa siyo ushetani

Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Ngusa Samike akizungumza na wajumbe wa kamati ya amani ya viongozi wa dini mkoa wa Mwanza wakati akifungua kikao cha mafunzo ya umuhimu wa sensa

Mwanza. Baadhi ya viongozi wa dini mkoani Mwanza wamewataka waumini wa dini mbalimbali nchini kujitokeza katika Sensa ya Watu inayotarajiwa kufanyika Agosti 23, 2022 huku wakisema maandiko matakatifu yanaitambua sensa na kwamba siyo mambo ya shetani kama inavyodhaniwa na baadhi ya watu.

Wito huo umetolewa leo Jumanne Juni 28, 2022 jijini Mwanza na Mwenyekiti wa Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini Mkoa wa Mwanza, Askofu Charles Sekelwa kwenye kikao cha mafunzo yanayohimiza umuhimu wa sensa kwa wajumbe wa kamati hiyo kutoka wilaya za Mkoa wa Mwanza.

Askofu Sekelwa amesema dini ya Kikristo inaikubali, kuithamini na kuifanyia kazi sensa na viongozi wa dini wana wajibu wa kuiambia jamii kuwa zoezi hilo ni sahihi huku akiitaka jamii kuepuka uvumi unaoenezwa ukihusisha Sensa na imani potofu kuwa ni haramu na si sahihi.

“Sensa inakubalika katika imani yetu ya Kikristo na maandiko matakatifu yanaiunga mkono usipokuwa na sensa utatawala gizani. Sisi viongozi wa kiroho tujitafutie maarifa sahihi tuwape elimu waumini wetu na tuache upotoshaji juu ya sensa kuwa ni mambo ya shetani,” amesema Askofu Sekelwa.

Naye Shehe Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Hassan Kabeke amesema kamati hiyo ni nyenzo muhimu ya kutumika katika kuwafikia wananchi na kuwapa elimu na taarifa iliyo sahihi juu ya sensa huku akisisitiza kuwa wanaosema sensa ni haramu wamechanganyikiwa.

“Takwimu zinazokusanywa kupitia sensa zinasaidia kuimarisha na kuboresha huduma kwa jamii, nchi na taasisi za dini hivyo ni wajibu wetu kujitokeza kikamilifu,” amesema Shehe Kabeke.

Akifungua kikao hicho, Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Ngussa Samike amewaomba viongozi wa dini nchini kushirikiana na serikali kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa sense, huku akizitaka taasisi mbalimbali nchini zikiwemo za dini kuweka mabango na matangazo yenye ujumbe wa Sensa kwenye nyumba za ibada na kutenga muda wa kuwapa elimu waumini wao.

“Tujitokeze kwa wingi tutoe taarifa sahihi zitakazosaidia kuufungua mkoa wetu, tuache kusikiliza wanaopotosha tuwe wa kwanza kuielimisha jamii tusiache wapotoshaji wachukue nafasi tuwaelimishe watu tuondoe hisia potofu zinazojengeka katika jamii zoezi hili ni la kwetu sote,” amesema Samike.

Akiwasilisha mada ya umuhimu wa sensa mbele ya wajumbe wa kamati ya amani, Mratibu wa sensa wilaya ya Nyamagana, Ruhinda Costantine amesema sensa hutumika kupanga na kufuatilia utekelezaji wa mipango ya maendeleo endelevu ya wananchi katika sekta zote kiuchumi, kijamii na mazingira ambapo Serikali hupanga bajeti inayokidhi matakwa ya wananchi na maeneo wanayoishi.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *