Viongozi wa Jumuiya ya SADC wahamasisha ukuaji uchumi na kilimo

Mkutano wa 42 wa viongozi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), ulimazilika jana katika mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo Kinshasa, huku wakuu wa jumuiya hiyo wakihamasisha ukuaji wa uchumi, kilimo na juhudi zaidi katika sekta ya madini.

Mkutano wa mwaka huu ulikuwa na kaulimbiu isemayo “kuhamasisha viwanda kupitia, usindikaji wa kilimo, faida ya madini, na mifumo ya thamani ya kikanda kwa kujumuisha wote na ukuaji stahamilivu.”

Masuala makuu katika kikao hicho yalijumuisha uzinduzi wa jopo la wakuu wa nchi na wawakilishi wa serikali waliohudhuria, wakifatiwa na utoaji wa medali kuwakumbuka na kuwapa heshima waanzilishi wa SADC.

Akihutubia mkutano huo, Rais Felix Tshisekkedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambaye pia ndiye mwenyekiti wa Jumuiya ya SADC alisema: “Nitahakikisha natekeleza mipango ya kuendeleza miundo mbinu na huduma katika ukanda ambayo inahusika moja kwa moja na mikakati yetu mikuu katika kuchochea maingiliano wa kiuchumi na kutokomeza umaskini katika ukanda wa SADC.”

Mkutano huu umefanyika wakati ambapo nchi mwenyeji inakabiliwa ghasia mpya upande wa mashariki mwa nchi. Mbele ya viongozi wenzake, Rais Felix Tshisekedi alishutuma vikali kile alichokitaja kuwa ‘uhuni na ukatili unaofanywa dhidi ya nchi yake na jirani yake Rwanda.

Baadhi ya mataifa wanachama wa SADC kama vile Malawi na Tanzania yanachangia wanajeshi katika kikosi maalumu cha ulinzi wa amani cha Umoja wa Mataifa MONUSCO.

Mwanachama mwingine wa SADC yaani Msumbiji pia inakabiliana na uasi wa wanamgambo katika majimbo ya kaskazini ambapo jumuiya hiyo imetuma wanajeshi pia katika nchi hiyo.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *