Polisi nchini Tunisia imewatia mbaroni viongozi kadhaa watajika wa upinzani nchini humo akiwemo Jaouhar Ben Mbarek mmoja wa wakosoaji wakuu wa Rais Kais Saied.
Dada wa kiongozi huyo wa upinzani ambaye ni mmoja wa viongozi wa ngazi za juu wa harakati ya upinzani ya National Salvation Front (NSFT) amewaambia waandishi wa habari kwamba, kaka yake ametiwa mbaroni na vyombo vya usalama.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, Issam Chebbi, kiongozi wa chama cha al-Jamhouri naye ametiwa mbaroni na anaendelea kushikiliwa na vyombo vya usalama.
Kamata kamata hiyo ya vyombo vya usalama dhidi ya wapinzani inaripotiwa katika hali ambayo, hivi majuzi Rais wa Kais Saied wa Tunisia aliamua kumpiga kalamu na kusitisha majukumu ya Waziri wa Ajira na Mafunzo, Nasreddine Nsibi, hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Rais huyo wa Tunisia.
Ikumbukwe pia kuwa, tarehe 7 mwezi huu wa Februari, Rais Saied alimfuta kazi Waziri wa Mambo ya Nje Othman Jerandi, mwezi mmoja baada ya kumfukuza kazini Waziri wa Biashara Fadhila Rabhi.
Mnamo Julai 25, 2021, Rais Kais Saeid, alipitisha maamuzi na kuchukua hatua kadhaa zisizo za kawaida ikiwemo kutangaza kufuta mamlaka ya Bunge, kuondolewa kwa kinga ya Wabunge, kumfuta kazi Waziri Mkuu na kuvunja tume ya usimamizi wa katiba, hatua ambazo zilizusha mtafaruku na mkwamo wa kisiasa nchini Tunisia, ambao uliambatana na wimbi la maandamano ya vyama na mirengo ya kisiasa, kikiwemo chama cha Kiislamu cha al-Nahdha.