Nchi maskini ya Kiarabu ya Yemen imesababishiwa hasara kubwa sana na madola vamizi yaliyoongozwa na Saudia katika vita vya miaka mingi nchini humo.
Hayo yamesemwa na Kitengo cha Biashara za Nje cha Wizara ya Viwanda na Madini ya Serikali ya Wokovu wa Kitaifa yenye makao yake San’a, mji mkuu wa Yemen ambacho kimesema kwenye taarifa yake kwamba, vita vya kivamizi vinavyoongozwa na Saudi Arabia vimeitia hasara ya dola bilioni 64 nchi hiyo ya Kiislamu.
Saudia kwa uungaji mkono kamili wa madola ya kibeberu hasa Marekani na kwa kushirikiana na baadhi ya nchi za Kiarabu hasa Muungano wa Falme za Kiarabu (Imarati) ziliianzisha vita vya kivamizi vya pande zote mwezi Machi 2015 na kuizingira nchi hiyo kutokea angani, ardhini na baharini.
Vita hivyo vya kivamizi vya Saudi Arabia na wenzake vimeshaua idadi kubwa ya wananchi wa Yemen na kujeruhi mamia ya maelfu ya wengine na kuwafanya wakimbizi zaidi ya watu milioni 4.
Televisheni ya Al Mayadeen imetangaza habari hiyo leo Jumanne na kuongeza kuwa, tangu vilipoanza vita vya kivamizi nchini Yemen, nchi hiyo imeshapata hasara ya dola bilioni 64071,2021.
Ripoti hiyo ya Wizara ya Viwanda na Madini ya Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen imesema, matatizo makubwa yanatokana na kuendelea kuzingirwa kila upande nchi hiyo na madola hayo vamizi hasa Saudi Arabia ambayo inazuia chochote kuingia na kutoka nchini Yemen na haiheshimu makubaliano yoyote ya kusitisha vita.