Sambamba na juhudi za Marekani za kuwa na ushawishi mkubwa zaidi katika nchi za Kiafrika, nchi hizo zinazidi kupoteza imani kwa viongozi wa White House siku baada ya siku.
Vyombo vya habari vimeripoti kuwa, wakati Marekani ikifanya mkutano na wakuu wa nchi za Afrika ili kukabiliana na ushawishi wa China na Russia bara humo, inaonekana kuwa nchi nyingi za Kiafrika haziamini tena ahadi za viongozi wa Marekani.
Washington imetoa ahadi nyingi kwa nchi za Afrika ambazo kamwe hazikutekelezwa suala ambalo limewafanya Waafrika kutafuta suluhisho mbadala la maendeleo ya ustawi wa watu wa bara hilo.
Ripoti zinasema nchi za Asia Magharibi na Afrika zimechoshwa na ahadi hewa za Marekani na washirika wake hadi nchi kama China zilipojitokeza na kuanza ushirikiano na nchi hizo katika masuala ya ustawi na maendeleo.
Ripoti zinaonesha kuwa, viongozi wa Marekani hawakujifunza kutokana na makosa yao na kutoka kwenye historia, na jambo la kusikitisha ni kwamba wanafanya mambo ambayo hayana faida kwa watu wa Afrika.
Katika baadhi ya vikao vyake wiki hii mjini Washington, Rais Biden ametoa matamshi yanayoingilia masuala ya ndani ya nchi za Afrika suala ambalo limekabiliwa na msimamo mkali wa nchi husika.
Kwa mfano tu, Rais Paul Kagame wa Rwanda ameikosoa vikali Marekani kwa kuishinikiza serikali ya Kigali imuachie huru Paul Rusesabagina, nyota wa filamu ya “Hotel Rwanda” aliyegeuka na kuwa mkosoaji mkubwa wa serikali ya Kigali.
Akizungumza mjini Washington pambizoni mwa Mkutano wa Marekani na Afrika, Kagame amesema Rwanda haitamruhusu yoyote kuishinikiza nchi hiyo kufanya jambo linalogusa maisha ya Wanyarwanda.
Rais Kagame amehoji, “Rwanda imuachie huru Rusesabagina kwa msingi gani? Kwa kuwa ni mashuhuri na ni mkazi wa kudumu wa Marekani?”
Septemba mwaka jana, Mahakama Kuu ya Rwanda ilimhukumu Rusesabagina kifungo cha miaka 25 jela baada ya kumpata na hatia ya kujihusisha na kundi la waasi linalotuhumiwa kuhusika na mashambulio ya umwagaji damu ya utumiaji bunduki na maguruneti katika miaka ya 2018 na 2019.
Itakumbukwa kuwa, kuanzia Jumanne wiki hii Rais wa Marekani, Joe Biden, alikuwa mwenyeji wa viongozi kutoka nchi za Afrika huko mjini Washington DC, huku White House ikifanya mikakati ya kupunguza pengo la ukosefu wa uaminifu kati ya Marekani na Afrika.