Mnamo 2020, Umoja wa Mataifa ulichapisha ripoti iliyofichua hatari ya wahamiaji wanaofanya kazi katika “mfumo wa kisasa wa chakula wa Italia”, ambao waliteswa na “kuachwa katika hali mbaya” bila hati. Kulingana na ushahidi, sio mengi yamebadilika.
Taarifa zinasema wahamiaji wa Kiafrika wanaovuna zeituni huko Sicily, Italia wanaishi bila maji ya bomba, maji taka au umeme, chombo kimoja cha habari cha Uingereza kiliripoti baada ya kutembelea “ghetto” ya wahamiaji karibu na mji wa Campobello di Mazara.
Wafanyakazi wanalipwa mshahara duni sana wa takribani dola mbili kwa saa kwa sababu hawana hadhi ya kisheria, na wameingizwa katika kazi hiyo kupitia mfumo wa genge unaojulikana kama “caporalato”, na maana yake ni kwamba wahamiaji hawafanyi kazi moja kwa moja kwa ajili ya wakulima.
Kila mwaka wakati wa mavuno ambayo huanza Septemba hadi Novemba, kambi ya wahamiaji hujazwa zaidi ya watu 1,000 bila karatasi rasmi, ambao wengi wao wanaripotiwa kutoka Gambia, Senegal na Tunisia.
Maisha katika kambi hiyo hayana usalama mkubwa kutokana na ripoti za visa vya biashara ya dawa za kulevya na biashara ya ngono. Mnamo 2021, moto uliharibu sehemu kubwa ya kambi, na kuua mtoto mchanga mhamiaji.
Mwezi Oktoba, maandamano yaliandaliwa na wahamiaji wa Kiafrika na wanaharakati wa Italia kuadhimisha kumbukumbu ya mwaka wa kwanza wa moto huo na kutoa wito wa hali bora kwa wale wanaoishi katika kambi.
Issa, mhamiaji wa Gambia aliyeshiriki maandamano hayo, alitoa maoni yake kuhusu kisa kingine cha kusikitisha. Mnamo 2021, mfanyakazi wa shamba kutoka Mali mwenye umri wa miaka 27 anayeitwa Camara Fantamadi, alikufa baada ya kuchuma nyanya wakati wa joto kali huko Puglia.
Hivi majuzi, Sicily ilisajili rekodi ya joto kali Ulaya ilipofika kiwango cha nyuzi joto 48. Kisiwa hicho cha Mediterania kwenye ncha ya kusini ya Italia kiko moja kwa moja katika kitovu cha mawimbi ya joto barani Ulaya yanayosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa.
Kulingana na Umoja wa Mataifa, kati ya wahamiaji 450,000 na 500,000 wasio wa kawaida wanafanya kazi katika sekta ya kilimo ya Italia.