Abiria wa reli ya Uingereza wametahadharishwa kuhusu kutatizika safari mwanzoni mwa mwaka mpya, huku wafanyakazi wa reli wakianzisha mgomo wa kwanza jana.
Uingereza sasa iko katika hali mbaya zaidi ya migomo ya wafanyikazi tangu Margaret Thatcher aingie madarakani miaka ya 1980, huku mfumuko wa bei ukifuatia zaidi ya miaka 10 ya ukuaji wa mishahara uliodorora, na kuwaacha wafanyakazi wengi kushindwa kujikimu.
Migomo ya mara kwa mara ya reli imelemaza mtandao huo katika miezi ya hivi karibuni huku wauguzi, wafanyakazi wa viwanja vya ndege, wahudumu wa afya na wafanyakazi wa posta pia wakijiunga na migomo, wakitaka malipo ya juu ili kuendana na mfumuko wa bei uliovunja rekodi ya miaka 40 na kukifika asilimia 10.7 mwezi Novemba.
Migomo katika majira ya baridi imeenea kote nchini Uingereza na hivyo kutoa pigo kwa maisha ya kila siku ya watu pamoja na uchumi wa nchi hiyo ambao tayari unasuasua. Migomo hiyo haionyeshi dalili ya kusimama mwanzoni mwa mwaka mpya huku wafanyakazi katika sekta nyingi wakidai malipo ya juu ili kuendana na kasi ya mfumuko wa bei.
Serikali ya Uingereza imepinga mapendekezo ya kuongeza mishahara na kutangaza kuwa haiwezi kumudu kuwapa wafanyakazi wa sekta ya umma ongezeko linalolingana na mfumuko wa bei.
Mick Lynch, mkuu wa chama cha wafanyakazi wa reli cha RMT, amesema serikali inaonekana kuridhika na mgomo huo uendelee.
“Pande zote zinazohusika zinajua nini kifanyike ili kupata suluhu, lakini serikali inazuia hilo,” Lynch amesema.
Waziri Mkuu wa Uingereza, Rishi Sunak, anasisitiza kuwa kupandisha mishahara kunaweza kuzidisha mfumuko wa bei, hata hivyo, wafanyakazi wanasisitiza kuwa wanataka mishahara iongezwe ili kuendana na mfumuko wa bei.