Shirikisho la Soka la Asia Magharibi (WAFF) limetoa mwito wa kusimamishwa utawala wa Israel katika mashindano na shughuli zote zinazohusiana na mpira wa miguu duniani, madhali Tel Aviv inaendeleza vita vya mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza.
Rais wa shirikisho hilo, Mwanamfalme Ali bin Hussein ametoa mwito huo katika barua ya wazi aliyoituma jana Alkhamisi kwa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), mashirikisho ya kandanda na kwa wanachama wa vyama vya mchezo huo kote duniani.
Sehemu ya barua hiyo inasema, “Unganeni nasi na mchukue msimamo madhubuti dhidi ya dhulma zinazofanyika Palestina, na jinai za kivita zinazoendelea kufanywa katika Ukanda wa Gaza.”
Mbali na kutaka kutengwa Shirikisho la Soka la Israel na kutoruhusiwa kushiriki katika shughuli zozote za soka madhali Tel Aviv inaendeleza mauaji ya kimbari Gaza, Rais wa WAFF ametaka wahusika wote waliotumiwa barua hiyo wakiwemo makocha, marefa, wachezaji na maafisa wa mashirikisho ya soka duniani kwa kauli moja walaani mauaji ya raia wasio na hatia wa Gaza, na uharibifu wa miundimbinu ya soka katika eneo hilo.
Haya yanajiri siku chache baada ya Aleksander Ceferin, Rais wa Muungano wa Mashirikisho ya Soka ya Ulaya (UEFA) kusema kuwa, kushiriki Israel na Ukraine katika fainali zijazo za michuano ya EURO 2024 ni hatari kwa usalama.
Alisema kushiriki Israel na Ukraine kwenye mechi za EURO 2024 kunaweza kuwa tishio la usalama kwa mashindano hayo ya kieneo yanayotazamiwa kufanyika katika msimu wa joto kali nchini Ujerumani.
Hii ni katika hali ambayo, chuki dhidi ya Wazayuni zimeongezeka kote duniani kufuatia vita vya utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.
Maandamano ya kulaani jinai hizo za Israel huko Gaza yamekuwa yakifanyika katika pembe zote za dunia, ikiwemo huko Ujerumani ambapo mashindano hayo ya kandanda yanatazamiwa kufanyika katika msimu wa joto kali.