Maafisa wa Nigeria wamethibitisha taarifa zinazosema kuwa, wafungwa 21 kati ya waliotoroka baada ya jela moja kushambuliwa na watu wenye silaha katika jimbo la Plateau la katikati mwa nchi hiyo, wamekamatwa na kurejeshwa jela.
Faraan: Kwa uchache watu 11 waliuwa na wafungwa 252 walitoroka baada ya watu wenye silaha kuivamia jela hiyo iliyoko katika mji wa Jos, makao makuu wa jimbo la Plateau. Watu wasiojulikana wenye silaha waliivamia jela hiyo tarehe 28 mwezi uliopita wa Novemba na kupelekea idadi kubwa ya wafungwa kukimbia.
Katika taarifa yake ya jana Jumanne, Kikosi cha Mafunzo cha Nigeria (NCoS) kimesema kuwa, baadhi ya wafungwa wamejisalimisha kwa maafisa husika kwa hiari yao wakiwemo wafungwa wawili ambao inasemekana walirejeshwa kwenye jela hiyo na mama zao.
Taarifa hiyo imesema, baadhi ya wafungwa hao wamekamatwa na maafisa usalama wa jimbo hilo katika msako maalumu ulioanza mara baada ya kuvmiwa jela hiyo.
Katika taarifa nyingine, Mohammed Tukuru, naibu mdhibiti mkuu wa kikosi cha NCoS ambaye ametembelea jela hiyo kutathmini hasara zilizosababishwa na watu hao wenye silaha amesema, kulitumika vifaa vya kisasa katika uvamizi huo.
Wakati jela hiyo iliposhambuliwa, ilikuwa na wafungwa 1,060 wakiwemo 560 walikuwa wanasubiri hukumu zao na 500 walikuwa wameshahukumiwa kifungo. Hayo yamesemwa na Francis Enobore, msemaji wa Kikosi cha Mafunzo cha Nigeria, (NCoS).
Mwezi Oktoba mwaka huu, serikali ya Nigeria ilisema kuwa, imeamua kufanya uchunguzi maalumu katika jela za nchi hiyo kuona uimara wa jela hizo hasa baada ya kutokea kesi kadhaa za kuvunjwa na kutoroka jela wafungwa katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni.