Wahadhiri wa vyuo vikuu Nigeria wahitimisha mgomo wao wa miezi 8

Muungano wa Kitaaluma wa Wafanyakazi wa Vyuo Vikuu vya Serikali Nigeria (ASUU) umetangaza leo Ijumaa kuhitimiha mgomo wao wa miezi 8.

ASUU ambayo ni taasisi mwavuli ya wahadhiri wa Vyuo Vikuu vya serikali kote Nigeria, imetoa taarifa hiyo leo katika mtandao wa kijamii. Hata hivyo bado haijabainika wazi ni lini masomo ya vyuo vikuu yaatanza tena rasmi nchini humo.

Uamuzi huu umetangazwa baada ya kufanyika mazungumzo ya kina kati ya taasisi ya ASUU na wawakilishi wa serikali ya Abuja katika mkutano ambao ulisimamiwa na wabunge kadhaa  wa bunge la wawakilishi mjini Abuja.

Emmanuel Osodeke, mkuu wa ASUU ameeleza kuwa wanapaswa kufanya kazi pamoja na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi  ili kumalizie vyema jambo walilolianzisha ili kila Mnigeria ajivunie kuwa na vyuo vikuu vya kujifaharisha. Ameahidi kwamba, katika siku zijazo hawataruhusu  mgomo kuendelea na kupindukia siku mbili.

Kabla ya tangazo hili la kuhitimisha mgomo wa miezi nane wa vyuo vikuu nchini NIgeria, duru kadhaa za mazungumzo kati ya wahadhiri na serikali zilishindwa kutatua mzozo huo. Mwezi uliopita mahakama iliwaagiza wahadhiri wa vyuo vikuu kuhitimisha mgomo huo; hata hivyo muungano wa ASUU ulikata rufaa dhidi ya uamuzi huo.

Mamilioni ya wanafunzi wa vyuo vikuu nchini Nigeria wamekuwa nyumbani tangu Februari 14 mwaka huu kama sehemu ya mlolongo wa migomo ya muda mrefu ya wahadhiri wa vyuo vikuu nchini humo. Nigeria ina vyuo vikuu vya serikali zaidi ya 100 na wanafunzi wanaokadiriwa kuwa milioni 2 na laki tano.

Wahadhiri hao waliogoma walikuwa wakitaka kuangaliwa upya kwa mazingira yao ya utendaji kazi ikiwa ni pamoja na vigezo ambavyo  serikali hutumia kuwalipa mishahara, kuboreshwa kwa ufadhili wa vyuo vikuu huku wakisisitiza kulipwa mishahara yao yote ambayo hawajalipwa tangu waanze mgomo.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *