Wairaqi wamkumbuka Shahidi Soleimani, waapa kuendeleza njia yake

Wananchi wa Iraq katika Mkoa wa Salahedine wameshiriki katika hafla ya kumkumbuka kamanda wa zamani wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) Qassem Soleimani na wenzake wakati wa kukaribia maadhimisho ya mwaka wa tatu wa kuuawa kwao shahidi katika hujuma ya jeshi la kigaidi la Marekani.

Wananchi pamoja na  maafisa wa kijeshi na serikali wamehudhuria kumbukumbu hiyo katika mji wa Dujail kaskazini mwa mji mkuu Baghdad kwa ajili ya kuenzi kumbukumbu za mashahidi, akiwemo Luteni Jenerali Soleimani na Abu Mahdi al-Muhandis, naibu mkuu wa Hashd Al-Shaabi au Jeshi la Kujitolea la Wananchi wa Iraq (PMF).

Katika hafla hiyo, washiriki wamewakumbuka makamanda hao waliopata ushindi katika vita dhidi ya ugaidi ambao walijitolea katika kuihami jamii ya Kiislamu na kukabiliana na njama za jinai za kundi la kitakfiri na kigaidi la Daesh na mabwana zao.

Viongozi wa Iraq walioshiriki katika hafla hiyo wamesisitiza umuhimu wa kuendeleza njia ya mashahidi. Jeshi la Marekani liliwaua makamanda hao wawili wenye ushawishi mkubwa na wenzao katika shambulio la ndege isiyo na rubani karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad mnamo Januari 3, 2020. Shambulizi hilo liliamriwa moja kwa moja na rais wa zamani wa Marekani Donald Trump.

Makamanda hao wawili wanatambulika duniani kote kwa mchango wao katika kulitokomeza kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh katika eneo hususan Iraq na Syria. Kundi hilo la kigaidi lilikuwa limefanya mashambulizi na jinai kubwa zaidi dhidi ya raia Waislamu na Wakristo tangu lilipoibuka katika nchi hizo mbili za Kiarabu.

Watu wa Iran na Iraq hufanya hafla za kila mwaka kukumbuka jukumu muhimu la makamanda hao wawili katika kuwaangamiza magaidi wa Daesh. Kabla ya kushindwa, Daesh ilikuwa imechukua udhibiti wa sehemu kubwa ya Iraq na Syria.

Mwaka 2014, wakati kundi la kigaidi la Daesh lilipoanzisha kampeni yake ya ugaidi nchini Iraq, washauri wa kijeshi wa Iran wakiongozwa na Jenerali Soleimani na baada ya kualikwa na serikali ya Iraq walielekea katika nchi hiyo jirani kwa msaada wa wanajeshi wa Iraq, na kuwasaidia hatimaye kukomboa maeneo yao yote kutoka kwa magaidi hao ambao walikuwa wanapata himaya ya Marekani. Mapigano dhidi ya magaidi wa Daesh au ISIS yalichukua muda wa miaka mitatu kumalizika.

Mwezi Novemba, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Seyed Ali Khamenei alisema kuwa jina la Jenerali Soleimani linaikasirisha Marekani na washirika wake.

Haj Qassem Soleimani alikuwa kielelezo cha sera ya Jamhuri ya Kiislamu katika kukabiliana na mipango ya adui. Alivuruga mpango wa kina wa adui,” alisema Kiongozi Muadhamu katika hotuba yake katika mkutano na Vikosi vya Kujitolea vya wananchi, Basij.

Iran na Iraq zimeunda kamati ya pamoja ya uchunguzi kufuatilia mauaji hayo kisheria. Kulingana na matokeo ya hivi punde ya timu ya wanasheria, watu 120 wametambuliwa kuhusika katika mauaji ya kigaidi ya Shahidi Soleimani, huku Trump akiongoza orodha ya wahalifu hao.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *