Makumi ya wananchi wa Jordan wamekusanyika mbele ya ubalozi wa utawala haramu wa Israel mjini Amman ambapo sambamba na kuulaani jinai za utawala haramu wa Israel wametangaza himaya na uungaji mkono wao kwa msikiti wa al-Aqswa.
Waandamanaji hao wakiwemo wajumbe wa vyama mbalimbali vya siasa na wanaharakati wa asasi na jumuiya mbalimbali za kiraia wamesisitiza umuhimu ulionao msikiti wa al-Aqswa na kutoa wito wa kuungwa mkono kibla hicho cha kwanza cha Waislamu.
Kadhalikka waandamanaji hao wametangaza kuunga mkono muqawama na mapambano ya wananchi madhulumu wa Palestina na kupiga nara za kulaani makubaliano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala dhalimu wa Israel unaotenda jinai kila uchao dhidi ya wananchi wa Palestina
Katika miezi ya hivi karibuni vitendo vya hujuma na uvamizi wa walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Wapalestina hususan katika Msikiti wa al-Aqswa vimeongezeka mno.
Vitendo vya kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu huko Palestina vinafanyika katika hali ambayo, viongozi wa nchi za Kiarabu na jamii ya kimataifa wameendelea kunyamaza kimya na kutochukua hatua zozote za maana za kukabiliana na vitendo hivyo vinavyokinzana na utu na ubinadamu.
Utawala wa Kizayuni ambao unaungwa mkono kikamilifu na Marekani katika hatua zake hizo haramu umedhamiria kubadilisha muundo wa kijiografia na kidemografia wa maeneo ya Palestina; ili kuyazayunisha maeneo hayo na kuhakikisha unazihodhi na kuzidhibiti kikamilifu ardhi za Wapalestina.