Wajumbe wa Baraza la Seneti wamtaka Biden aache kuipatia Israel msaada wa silaha

Wajumbe wa Baraza la Seneti la Marekani wamemuandikia barua Rias wa nchi hiyo Joe Biden wakimtaka aache kuipatia silaha Israel ambayo imekuwa ikifanya mauaji dhidi ya raia katika Ukanda wa Gaza huko Palestina.

Duru za karibu na Seneti ya Marekani zinasema kuwa, wawakilishi 7 wa baraza hilo kutoka chama cha Kidemokrasia na Bernie Sanders mwakilishi wa kujitegemea wa jimbo la Vermont wamemuandikia barua Biden na kumtaka asitishe mara moja misaada ya kijeshi kwa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Wajumbe hao wamesema katika barua hiyo kwamba, Joe Biden anapaswa kumueleza wazi na bayana Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa Israel kwamba, kutofika misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza kutakuwa na matokeo mabaya sana.

Pia wamesisitiza kwamba, hatua za Netanyahu zinakiuka kifungu cha himaya na uungaji mkono wa kibinadamu katika Sheria ya Misaada ya Kigeni ya Marekani.

Katika matamshi yanayokinzana na kugongana, Rais wa Marekani amelitaja shambulio la Israel dhidi ya Rafah, kusini mwa Gaza, kuwa ni “mstari mwekundu” ambao haupaswi kuvukwa, lakini wakati huo huo amesema kwamba, hana mstari mwekundu katika kuuunga mkono utawala wa Kizayuni na kwamba ni muhimu sana kuulinda utawala huo.

Biden amesisitiza kuwa, kuhusu mstari mwekundu wa Washington kwa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amesema kuwa kuilinda Israel ni jambo muhimu na hakuna mstari mwekundu wa kuacha kutuma silaha kwa utawala huo.

Kimsingi ni kuwa, tangu kuanza kwa vita vya Israel katika Ukanda wa Gaza, Marekani imekuwa muungaji mkono mkuu wa utawala ghasibu wa Israel na imeipatia Tel Aviv msaada mkubwa wa kisiasa, kiuchumi, kijeshi na silaha.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *