Dar es Salaam. Siku moja baada ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kukemea tabia ya watumishi wa afya kutekeleza wagonjwa, Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania (TNMC) limewasimamisha kazi wakunga wawili kwa kosa kutelekeza wajawazito na kusababisha madhara kwa akina mama waliofika kujifungua.
Watumishi hao ni pamoja John Chuma wa Zahanati ya Boheloi iliyopo Lushoto, Tanga na Maclina Gwido Mduda wa Zahanati ya Mtibwa iliyopo Manispaa ya Sumbawanga, Rukwa.
Hatua hiyo imekuja siku nne baada ya baraza hilo kumsimamisha kazi kwa miezi mitatu, muuguzi wa mkunga wa Zahanati ya Kashai iliyopo Manispaa ya Bukoba, Leticia Kokutebesa Muganyizi kwa kosa la kutelekeza akina mama wajawazito.
Taarifa iliyotolewa leo Jumatano Julai 6, 2022 na Msajili wa Baraza hilo, Agnes Mtawa imeeleza kuwa kwa nyakati tofauti wakunga hao walishindwa kuzingatia maadili na miongozo ya kitaaluma wakati wa kutoa huduma na kusababisha madhara kwa akina mama waliofika kujifungua.
“Baraza limesikitishwa na linalaani vitendo vilivyofanywa na wauguzi na wakunga hao kukiuka sheria ya uuguzi na ukunga ya mwaka 2010 kifungu cha 25 (2)(a) na (3)(f)(k) pamoja na kanuni na misingi ya maadili ya kitaaluma ya wauguzi na wakunga Tanzania kwamba ni marufuku kumtelekeza mgonjwa, mgonjwa anapaswa kupata huduma salama, zenye ubora na staha.
“Kwa mamlaka niliyokabidhiwa kwa mujibu wa kanuni 7(1) ya Fitness’ to practice, nawasimamisha kutoa huduma za uuguzi na ukunga, kuanzia leo Julai 6, 2022 kwa muda wa miezi mitatu wakati mashauri yao yakishughulikiwa na baraza kisheria na kitaaluma,” amesema Mtawa.
Amesisitiza kuwa baraza litaendelea kuchukua hatua kwa wale wote watakao kiuka maadili na miongozi popte walipo ikiwemo kuwafutia usajili na kuwanyang’anya leseni zinazowaruhusu kutoa huduma za uuguzi na ukunga nchini.
Akizindua jengo la kutolea huduma ya afya ya mama na mtoto katika Hospitali ya CCBRT jana Jumanne Julai 5, 2022 Rais Samia aliwataka wauguzi nchini kuacha dharau kwa wakina mama wajawazito ili kuwaepushia vifo vinavyoweza kuzuilika.
Alisema takwimu zinaonyesha asilimia kubwa ya wanaofariki ni kutokana na mapungufu ya wanaotoa huduma, ikiwemo upungufu wa weledi au dharau ya watoa huduma na usimamizi hafifu.
“Hii inanikumbusha kesi iliyotokea juzi Bukoba, ambapo wakina mama wawili wamekwenda kupata huduma ya kujifungua hospitali, anaambiwa mlinzi awaite manesi, anawajibu nesi kasema nisifungue mlango.
“Anaambiwa kuna wakina mama wanataka kujifungua, anajibu nesi amesema nisifungue mlango, mpaka wakina mama wamejifungulia getini, wengine wamekimbizwa walipokimbizwa.
“Kwa hiyo dharau hizi, uzembe huu, kutokuwa na usimamizi wa kutosha kunaleta maafa kwa wanawake wakati wa kujifungua,”alisema.
Jumamosi, Juni 2 ilielezwa kuwa Leticia Kokutebesa pamoja na mhudumu walikataa kuwafungulia mlango akina mama wajawazito wawili waliofika kujifungua nyakati za usiku kwa madai ya kuhofia usalama wao.