Wakuu wa masuala ya usalama wa Ethiopia na Kenya wajadili mapambano ya pamoja dhidi ya ugaidi

Maafisa wakuu wa masuala ya kiusalama wa Ethiopia na Kenya wamesisitizia haja ya kushirikiana zaidi na kufanya kazi kwa pamoja katika kukabiliana na ugaidi.

Shirika la Habari la Ethiopia limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, ujumbe wa Kenya, ukiongozwa na mkuu wa intelijensia, Jenerali Nuredin Mohammed Haji, umekwenda katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa na kukutana na mkuu wa Idara ya Taifa ya Ujasusi na Usalama ya nchi hiyo (NISS) Redwan Hussien.

Pande hizo mbili zimeazimia kuimarisha operesheni za pamoja ili kuzuia na kukabiliana na tishio linaloendelea la magenge ya kigaidi katika eneo hilo, hasa Jeshi la Ukombozi la Oromo (OLA) ambalo linaendesha shughuli zake kwenye mpaka wa Kenya na Ethiopia.

Kwa mujibu wa ofisi ya kijasusi ya Ethiopia, mazungumzo hayo yamehusu tishio linaloongezeka la genge la OLA, hasa utekaji nyara wake wa hivi karibuni wa raia wawili wa Korea Kusini ambao baadaye walikabidhiwa kwa genge jingine la kigaidi la al-Shabaab.

Ofisi hiyo pia imebainisha kuwa OLA ni genge lililoasi la chama cha upinzani kilichopigwa marufuku na linahusishwa na msururu wa vitendo vya uhalifu, vikiwemo utekaji nyara, uporaji, uharibifu wa mali na uchimbaji madini kinyume cha sheria.

Genge hilo la wabeba silaha linalalamikia kuwa watu wa Oromo wametelekezwa licha ya kwamba ndilo kabila kubwa zaidi nchini Ethiopia, lenye wastani wa watu milioni 35.

Wakuu hao wa kijasusi wa Kenya na Ethiopia pia wamesisitizia haja ya kutatuliwa kwa amani mzozo na ukosefu wa utulivu nchini Sudan.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *