Katibu Mkuu katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Kenya, Karanja Kibicho amesema kuwa, takriban Wakuu wa Nchi 20 wanatarajiwa kuwasili nchini Kenya kushiriki katika sherehe za kuapishwa Rais mteule William Ruto kesho Jumanne.
Kibicho alitoa tangazo hilo Jumamosi wakati Kamati ya Makabidhiano ya Madaraka ilipotembelea Uwanja wa Kasarani katika mji mkuu, Nairobi, ambapo ndipo sherehe hizo zinapotarajiwa kufanyika. Hata hivyo hakusema ni viongozi gani hasa watashiriki kwenye sherehe hizo.
Pia amesema, takriban watu 60,000 wataruhusiwa kuingia katika viwanja hivyo kushuhudia kuapishwa kiongozi mpya wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Serikali ya Kenya tayari imeitangaza Jumanne kuwa mapumziko ya kitaifa kuruhusu umma kuhudhuria sherehe hizo.
Ruto alimshinda Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga katika uchaguzi wa Agosti 9 katika kinyang’anyiro cha kumrithi Uhuru Kenyatta, ambaye amemaliza mihula miwili ya uongozi iliyoidhinishwa na katiba.
Odinga alipinga ushindi wa Ruto katika Mahakama ya Juu ya Kenya, lakini jopo la majaji saba wa mahakama hiyo liliidhinisha matokeo yaliyotangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka IEBC.
Mbali na Ruto, Rigathi Gachagua pia ataapishwa kuwa Naibu Rais mpya wa Kenya. Gachagua alikuwa mgombea mwenza wa William Ruto katika uchaguzi wa Agosti 9.ke