Walimwengu waendelea kutoa mwito wa kuwepo taifa huru la Palestina

Viongozi mbalimbali wa dunia wametoa miito ya usitishwaji vita katika Ukanda wa Gaza na kuwepo kwa suluhisho la mataifa mawili ya Israel na Palestina na kusema kuwa hiyo ndio njia pekee ya kuwepo amani ya kudumu eneo hilo.

Utawala haramu wa Israel ambao umeapa kuitokomeza Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS, imetupilia mbali miito ya uwepo wa taifa huru la Palestina na kusema utaendelea kuwa na udhibiti wa usalama huko Gaza hata baada ya vita hivyo kumalizika.

Mshirika wake mkuu, Marekani na nchi nyingine kadhaa, wamependekeza kwamba suluhisho la mataifa mawili ndio njia pekee ya kuhakikisha usalama wa kudumu wa pande zote.

Kabla ya mkutano na wajumbe wa Israel na Palestina, Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell amesisitiza juu ya suluhisho la mataifa mawili na kusema Israel haiwezi kudumisha amani kwa kwa mtutu wa bunduki. Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock amesema uwepo wa mataifa mawili ya Israel na Palestina ndio suluhu pekee katika mzozo huo wa Mashariki ya Kati.

Mawaziri 27 wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya watakutana na waziri wa mambo ya nje wa Israel Israel Katz, kabla ya kuzungumza na mwanadiplomasia mkuu wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina Riyadh al-Maliki. Mawaziri wa mambo ya nje wa Misri, Jordan na Saudi Arabia pia watafanya mazungumzo na mawaziri hao wa Ulaya.

Wapalestina kwa upande wao hususan harakati za muqawama huko Palestina zimekuwa zikisisitiza kuwa, njia pekee ya utatuzi wa kadhia ya Palestina ni kuendelezwa mapambano dhidi ya utawala ghasibu wa Israel unaotenda jinai kila leo dhidi ya Wapalestina.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *