“Walimwengu wamekuwa watazamaji tu wa jinai za Saudia dhidi ya Wayamen”

Kituo cha Haki za Binadamu cha Yemen cha Ainu Yemen (Jicho la Yemen) kimetoa radiamali yake kuhusiana na jinai mpya za muungano vamizi unaoongozwa na utawala wa Saudi Arabia na kutangaza kuwa, jamii ya kimataifa imeamua kuwa mtazamaji tu wa jinai zinazofanywa na Aal Saud na washirika wake huko nchini Yemen.

Kituo hicho sambamba na kulaani mashambulio ya mizinga ya Saudia na washirika wake katika maeneo mbalimbali ya mji wa Sa’dah kimeshangazwa mno na jinsi jamii ya kimataifa ilivyoamua kukunja mikono nyuma na kuwa mtazamaji wa jinai zinazofanywa kila leo dhidi ya wananchi wasio na hatia wa Yemen.

Sehemu nyingine ya taarifa ya Kituo cha Haki za Binadamu cha Yemen cha Ainu Yemen (Jicho la Yemen) imesema: Tunalaani vikali kimya cha jamii ya kimataifa kinara wao ukiwa Umoja wa Mataifa kutokana na kuamua kuwa mtazamaji tu wa unyama na jinai zinazofanywa na Saudi Arabia na washirika wake huko Yemen.

Saudi Arabia, kwa uungaji mkono wa Marekani, Muungano wa Falme za Kiarabu na nchi nyingine kadhaa, ulianzisha hujuma za kijeshi dhidi ya Yemen tangu mwezi Machi mwaka 2015 na kuiwekea vikwazo nchi hiyo vya nchi kavu, baharini na angani.

Ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwa, takriban raia 6,000 wa Yemen wamepata ulemavu kutokana na mashambulizi ya muungano wa Saudia, na kakthari miongoni mwao ni watoto wadogo.

Hujuma ya kijeshi ya Saudia na washirika wake mbali na kusababisha maafa imeharibu kabisa miundombinu katika nchi hiyo ambayo sasa inakabiliwa na maafa ya kibinadamu kutokana na wakazi wake kutopata huduma muhimu za chakula, maji na tiba.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *