Makumi ya walowezi Waisraeli wamevamia eneo la Msikiti wa al-Aqsa huko Quds (Jerusalem) Mashariki inayokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel, katika hatua nyingine ya uchochezi dhidi ya waumini Waislamu wa Kipalestina.
Walioshuhudia wanasema kwamba uvamizi wa walowezi hao wenye itikadi kali ulifanyika chini ya ulinzi mkali kutoka kwa wanajeshi wa utawala ghasibu wa Israel. Walowezi hao waliinua bendera za utawala haramu wa Israel na kucheza ngoma za uchochezi ndani ya eneo hilo.
Vikosi vya utawala vamizi wa Israel pia viliweka askari ndani na nje ya msikiti ili kulinda uvamizi wa walowezi hao.
Wanajeshi wa Israel pia waliwashambulia maelfu ya Wapalestina, wakiwemo vijana, katika eneo la la Bab al-Amoud la Msikiti wa Al Aqsa. Walijaribu kuwalazimisha Wapalestina kuondoka eneo hilo ili kuwaruhusu Wazayuni wakoloni kulitembelea. Uchochezi huo uliibua ghasia kufuatia malalamiko makalai ya Wapalestina.
Wakati huo huo, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, ilitoa wito kwa Wapalestina kutoka matabaka yote ya maisha kukusanyika kwa wingi, kuongeza uwepo wao katika eneo la msikiti huo, na kulinda eneo takatifu dhidi ya uvamizi wa mara kwa mara wa walowezi wa Israel.
“Tunawapongeza watu wa Palestina katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na katika Ukingo wa Magharibi ambao wanasimama kidete kupinga ukiukaji wa uvamizi wa Israel na uhalifu,” ilisema taarifa yake.
Hamas pia iliutaka Umma wa Kiarabu na Kiislamu, pamoja na watu huru wa dunia, “kuunga mkono uthabiti wa watu wa Palestina na kufanya kazi katika kuwalinda dhidi ya ukiukaji wa uvamizi wa Israel.”