Makumi ya walowezi wa Kizayuni wamefanya hujuma na mashambulio dhidi ya nyumba za Wapalestina katika kitongoji cha al-Laban kusini mwa mji wa Nablos kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Hujuma na mashambulio hayo ya walowezi wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina ambapo walikuwa wakisaidiwa na kupata himaya ya jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel huko katika mji wa Nablos yamefanyika usiku wa kuamkia leo.
Katika hujuma hiyo, walowezi hao wabaguzi wa Kizayuni wameharibu mali na milki za Wapalestina wa eneo hilo.
Hayo yanaripotiwa katika hali ambayo, hivi karibuni, mabuldoza ya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel yalivamia maeneo ya kaskazini mwa mji wa Quds na kuharibu mali na miliki za Wapalestina katika maeneo hayo.
Wanajeshi wa Israel wakiongozwa na mabuldoza walivamia kitongoji kimoja jirani na kivuko cha Qalandiya kaskazini mwa Quds inayokaliwa kwa mabavu na kuharibu mali na miliki kadhaa za Wapalestina.
Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) imesema katika ripoti yake kwamba, vitendo vya ukandamizaji vinavyofanywa na Israel vimeshadidi mno tangu kuanza mwaka huu wa 2021.
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, mwaka uliopita wa 2020 utawala wa Kizayuni wa Israel ulibomoa nyumba karibu 689 katika Ukingo wa Magharibi na Quds tukufu na kulazimisha mamia ya familia za Wapalestina kuwa wakimbizi.