Harakati inayopinga dhulma na ukandamizaji wa utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina imekosoa vikali undumakuwili wa nchi za Magharibi kuhusu vita nchini Ukraine kwa upande mmoja na katika Ukanda wa Gaza, huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu kwa upande mwingine.
Harakati ya Kimataifa ya Kuususia Utawala haramu wa Israel BDS katika taarifa jana Jumamosi ilieleza kuwa, Marekani, Ulaya na vile vile nchi za Kiarabu zilizoanzisha uhusiano wa kawaida na Israel ni washirika wa utawala wa Tel Aviv katika jinai zake dhidi ya wananchi wa Palestina.
Harakati hiyo imetoa mwito wa kususiwa utawala wa Kizayuni kutokana na mauaji ya halaiki na jinai dhidi ya wananchi wa Palestina wasio na ulinzi katika Ukanda wa Gaza ulio chini mzingiro.
Taarifa ya harakati hiyo imeongoza kuwa, Marekani, Uingereza, Umoja wa Ulaya na madola ya Kiarabu yaliyoanzisha uhusiano na Tel Aviv ni washirika wa Israel katika jinai zake dhidi ya taifa la Palestina, kupitia kuanzisha miungano na kiusalama na kijeshi na utawala huo haramu, sanjari na kuwasaliti Wapalestina.
Kadhalika harakati hiyo inayoshajiisha kususiwa, kutowekeza na kuwekewa vikwazo Israel imewataka wakazi wa Gaza kuendeleza mapambano yao dhidi ya uvamizi na mauaji dhidi ya mamia ya Wapalestina wakiwemo watoto wadogo, mkabala wa kimya cha muungano wa Magharibi na Waarabu.
Harakati ya Kimataifa ya Kuususia Utawala haramu wa Israel BDS imesema kimya cha Wamagharibi na madola ya Kiarabu kimeishajiisha Israel iendelee kutenda jinai za kutisha dhidi ya Wapalestina.
Imesisitiza kuwa: Undumakuwili wa Magharibi katika mgogoro wa kijeshi nchini Ukraine na vita vya kikatili vya Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza unaumiza na kughadhabisha.