Wamarekani: Ndani ya miaka 10 ijayo vita vya wenyewe kwa wenyewe vitatokea nchini

Matokeo ya uchunguzi mpya wa maoni yanaonyesha kuwa zaidi ya 40% ya Wamarekani wanaamini kwamba ndani ya miaka 10 ijayo, vita vya wenyewe kwa wenyewe vitatokea nchini humo.

Kugunduliwa hati zaidi ya 300 zenye muhuri wa siri kwenye nyumba ya rais wa zamani wa Marekani Donald Trump kumeshadidisha mvutano kati ya serikali ya Wademocrat na Trump mwenyewe na pia na maafisa wa chama chake cha Republican.
Kwa mujibu wa toleo la leo Jumanne la gazeti la Guardian, matokeo ya uchunguzi wa maoni uliofanywa kwa pamoja na taasisi ya uchunguzi wa maoni ya Uingereza ya YuGov na jarida la Economist yanaonyesha kuwa asilimia 43 ya Wamarekani wanaamini, upo uwezekano kwa kiwango fulani wa kutokea vita vya wenyewe kwa wenyewe ndani ya nchi hiyo katika miaka 10 ijayo.
Miongoni mwa wafuasi wakereketwa wa chama cha Democratic na watu wasio na vyama, kiwango hicho kimepungua hadi 40%, huku 56% ya Warepublican wakiwa wanaamini kwa kiwango fulani kwamba vita vya wenyewe kwa wenyewe vitatokea ndani ya miaka 10 katika nchi hiyo.

Kwa mtazamo wa 65% ya waliohojiwa katika utafiti huo uliofanywa na taasisi ya YuGov na jarida la Economist, ghasia za kisiasa zimeongezeka nchini Marekani katika miaka 10 iliyopita, na 62% wanaamini kuwa zitaongezeka katika miaka michache ijayo.

Katika mahojiano aliyofanyiwa hivi karibuni na televisheni ya Fox News, Seneta wa chama cha Republican kwa jimbo la Carolina Kusini, Lindsey Graham amekosoa kile alichokiita undumakuwili katika kuamiliana na rais wa zamani Trump na kuonya kuwa, iwapo Donald Trump atashtakiwa kwa kuziondoa Ikulu ya White House nyaraka za siri na za siri za kiwango cha juu kabisa na kugunduliwa nyumbani kwake, uasi na machafuko yatazuka katika mitaa ya nchi hiyo.
Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *