Wamarekani waandamana kulalamikia mauaji ya raia mweusi yaliyofanywa na askari polisi

Wananchi wa mji wa Memphis nchini Marekani wameingia barabarani kupinga na kulalamikia mauaji ya raia mweusi yaliyofanywa na polisi wa nchi hiyo.

Tyree Nichols, raia mweusi mwenye umri wa miaka 29, alikamatwa na kupigwa vibaya na polisi mnamo Januari 7 kwa madai ya kuendesha gari kihuni na kwa fujo. Alifariki baada ya kuwahishwa hospitali.
Mamlaka za Marekani zimewashtaki askari watano wa polisi kwa kosa la mauaji ya daraja la pili kwa kumpiga na kumjeruhi raia huyo mweusi katika jimbo la Tennessee.
Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran IRIB limeripoti kuwa, kufuatia kusambazwa picha za televisheni zinazohusiana na mauaji ya Tyree Nichols, jiji la Memphis nchini Marekani, limegeuka uwanja wa maandamano ya kupinga mauaji ya raia huyo mweusi yaliyofanywa na polisi.

Watu wenye hasira katika jiji hilo wamelalamikia miamala ya kikatili ya polisi wa Marekani, hasa katika kuamiliana na watu weusi.

Takwimu mpya za kundi liitwalo “Mapping Police Violence” linalofuatilia ukatili unaofanywa na polisi zinaonyesha kuwa katika mwaka uliomalizika wa 2022 polisi wa Marekani waliwaua watu 1,176.
Wataalamu wanasema, takwimu hizo ni kiashiria cha ongezeko la unyanyasaji unaofanywa na polisi wa Marekani dhidi ya watu weusi kwa sababu watu weusi ni 13% tu ya watu wote wa Marekani.
Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *