Makumi ya maelfu ya watu wamefanya maandamano katika majimbo na miji mbalimbali ya Marekani ukiwemo mji mkuu Washington, kushinikiza kuangaliwa upya sheria inayoruhusu kuuzwa na kumiliki silaha za moto kiholela nchini humo; siku chache baada ya kujiri mauaji ya kutisha huko Texas, ambapo watoto 19 wa shule na walimu wawili waliuawa kwa kufyatuliwa risasi.
Wanaharakati waliohutubia waandamanaji jijini Washington DC wamewataka Maseneta wa nchi hiyo ambao wanaonekana kuwa kikwazo cha kuangaliwa upya sheria hiyo ya kubeba bunduki, na kuchukua hatua mwafaka au wapigiwe kura ya kutimuliwa ofisini.
Meya wa Wilaya ya Columbia, Muriel Bowser ameuambia umati wa waandamanaji kuwa, “Tumechoka sasa! Nazungumza kama Meya, mama, na kama mmoja wa mamilioni ya Wamarekani wanaotaka Kongresi itekeleze majukumu yake, na jukumu lao kubwa ni kutulinda na kuwalinda watoto wetu kutokana na ukatili wa bunduki.”
Kwa mujibu wa vuguvugu la vijana la March for Our Lives, maandamano 450 kama hayo ya Washington yalifanyika pia hiyo jana katika miji ya New York, Los Angeles na Chicago.
Uuzaji na umiliki holela wa bunduki ni moja ya sababu kuu za mauaji ya utumiaji silaha moto nchini Marekani. Kwa wastani, ukatili wa utumiaji bunduki unaigharimu Marekani dola bilioni 229 kila mwaka.
Takwimu zinasema kuwa, kwa mwaka makumi ya maelfu ya watu huuawa au kujeruhiwa nchini Marekani kwa kupigwa risasi, nchi ambayo karibu bunduki milioni 270 ziko mikononi mwa raia.