Wamauritania watoa wito wa kususiwa bidhaa za Uswidi baada ya kuvunjiwa heshima Qur’ani

Wananchi wa Mauritania wametoa wito wa kukatwa uhusiano kati ya nchi za Kiislamu na Uswidi kupinga kutendo cha kuvunjiwa heshima Qur’ani Tukufu.

Ni baada ya vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu siku za Jumamosi na Jumapili iliyopita katika nchi Uswidi na Uholanzi, ambapo watu wenye misimamo mikali walivunjia heshima na kuchoma moto nakala ya Qur’ani Tukufu hususan mbele ya Ubalozi wa Uturuki mjini Stockholm, katika kitendo ambacho kiliidhinishwa na kusimamiwa na polisi nchini humo.

Kuvunjiwa heshima Qur’ani Tukufu kumezusha wimbi la hasira na malalamiko makali katika ulimwengu wa Kiislamu ambapo watetezi wa uhuru wa itikadi pia wamelaani vikali kuchomwa moto nakala ya kitabu hicho kitakatifu.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Anatolia, Waislamu wa Mauritania wameandamana mjini Nouakchott kupinga kitendo cha kuchomwa moto nakana ya Qur’ani nchini Uswidi na kuzitaka nchi za Kiislamu kuvunja uhusiano wao na Stockholm.

Waandamanaji hao walibeba vitambaa na mabango yenye maandishi kama vile “Matukufu Yetu ni Mstari Mwekundu”, na “Susia Bidhaa za Uswidi”. Vilevile wameyataka mataifa ya  dunia kususia bidhaa zote zinazotengenezwa nchini Uswidi.

Kufuatia kuchomwa moto Qur’ani huko Stockholm, mkuu wa kituo cha elimu cha wanazuoni wa Kiislamu nchini Mauritania ametoa fatwa na kutangaza: Ni wajibu kwa Waislamu kususia bidhaa zote za Uswidi, na marufuku hii itaendelea hadi serikali ya Stockholm itakapoomba msamaha kwa kuivunjia heshima Qur’ani Tukufu.

Siku chache zilizopita pia Kituo cha Kiislamu cha Al-Azhar nchini Misri kilitoa wito wa kususiwa bidhaa za Uswidi na Uholanzi ili kukabiliana na vitendo viovu vya kuvunjiwa heshima Qur’ani Tukufu katika mataifa hayo ya Ulaya.

Ijumaa ya jana pia mamilioni ya Waislamu wa Iran walifanya maandamana baada ya Swala ya Ijumaa kote nchini wakilaani vitendo vya kuvunjiwa heshima Qur’ani Tukufu katika nchi za Ulaya.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *