Wanajeshi 176 wa Marekani walijiua mwaka 2021

Idadi ya askari wanaojiua katika Jeshi la Marekani imezidi kuongezeka mwaka uliopita wa 2021 ambapo takwimu zinaonyesha kuwa askari 176 walijiua.

Takwimu hizo za Wizara ya Ulinzi ya Marekani, Pentagon, zinaonyesha kuwa, jeshi hilo limekuwa likijaribu kutafuta njia za kuimarisha kiwango cha maisha ya askari ili kuboresha afya yao ya kiakili.

Tovuti ya military.com pia imeandika kuwa kuna idadi kubwa ya askari wanaojiua katika Gadi ya Kitaifa ya Marekani  ambapo maafisa 102 wa kikosi hicho walijiua mwaka 2021. Aidha Gadi ya Kitaifa ya Anga ilitangaza maafisa wake 15 walijiua mwaka jana.

Hayo yanajiri wakati ambao data mpya zinaonyesha kuna ongezeko kubwa la hujuma za kijinsia katika Jeshi la Marekani ambapo mwaka 2021 kuliripotiwa ongezeko la asilimi 25.6 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia.

Mwaka jana pia utafiti mpya ulifichua kuwa, idadi ya askari wa Marekani na maveterani wa jeshi wa nchi hiyo wanaoaga dunia kwa kujitoa uhai ni mara nne zaidi ya wanajeshi wa dola hilo la kibeberu wanaouawa vitani katika vita vinavyoanzishwa na Washington kila uchao tokea Septemba 11 mwaka 2001.

Inaonekana kuwa, suala hilo la kujiua kwa wingi wanajeshi wa Marekani hususan wale walioshiriki katika vita vya Afghanistan na Iraq ni miongoni mwa matunda ya vita visivyo na ukomo vya watawala wa Marekani katika maeneo mbalimbali ya dunia kwenye miongo miwili iliyopita.

Mbali na hayo, maelfu ya wanajeshi wa Marekani walioshiriki katika vita vya Afghanistan na Iraq na kuendeleza uvamizi wa Washington katika nchi hizo wanasumbuliwa na aina mbalimbali za matatizo na magonjwa ya kiakili na kinafsi, na pale wanaporejea makwao huonekana kuwa na mienendo ya ajabu na isiyofaa kwa watu wa familia zao na katika jamii na hatimaye huamua kujitoa uhai kwa kujiua wenyewe baada ya kushindwa kustahamili adhabu na matatizo mengi ya kinafsi na kiakili.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *