Wanajeshi saba wa serikali ya Somalia wameuawa katika shambulio la jana Ijumaa lililofanywa na genge la ukufurishaji la al Shabab kwenye kambi ya kijeshi ya mji wa Somalia uliookombolewa na jeshi la Serikali wiki hii.
Wizara ya Habari ya Somalia imetangaza habari hiyo na kusema kuwa, kamanda mkuu wa kijeshi ni miongoni mwa waliouawa baada ya magaidi hao kuvamia kambi hiyo huko Galcad, mji ulioko katikati mwa Somalia yapata kilomita 375 kaskazini mwa mji mkuu Mogadishu.
Taarifa hiyo imesema pia kwamba, zaidi ya magaidi 100 wa al Shabab wameuawa baada ya wanajeshi kujibu shambulizi hilo la kushtukiza.
“Kulikuwa na mapigano makali huko ambapo magaidi walishindwa,” taarifa ya jana Ijumaa ya wizara hiyo imesema na kuongeza kuwa, “eneo hilo sasa liko chini ya udhibiti kamili wa vikosi vya Somalia.”
Al Shabab wametangaza kuwa wao ndio waliohusika na shambulio hilo, wakidai kukwa, wapiganaji wao walivamia kambi hiyo na kuua zaidi ya wanajeshi 150. Madai hayo lakini hayajathibitishwa.
Abdilahi Rage, mkazi wa mji wa Galcad, ameliambia shirika la habari la AFP kwa simu kwamba: “Washambuliaji wa Shabaab waliripua malori mawili yaliyokuwa na mabomu kabla ya mapigano ya ana kwa ana kuanza.”
Siku ya Jumanne, nagaidi wa al Shabab walifanya shambulio baya dhidi ya kambi ya kijeshi katika sehemu nyingine ya katikati mwa Somalia, siku moja tu baada ya serikali kusema imepata “ushindi wa kihistoria” dhidi ya magaidi hao kwa kuuteka mji wa kimkakati wa pwani wa Haradhere pamoja na Galcad.