Mabaki ya wanajeshi wa Ufaransa waliondoka nchini Mali jana Jumatatu, kuashiria mwisho wa Operesheni ya Barkhane katika nchi hiyo ya eneo la Sahel barani Afrika.
Taarifa ya Vikosi vya Jeshi la Ufaransa imesema, askari wa mwisho wa kikosi cha Barkhane waliokuwa katika ardhi ya Mali wameondoka na kuvuka mpaka baina ya nchi hiyo na Niger.
Sambamba na kuendelea kwa mvutano kati ya Ufaransa na Mali, hatimaye Paris imetangaza ukomo wa kuwepo kwa vikosi vya askari wa nchi za Ulaya vinavyojulikana kama Takuba, nchini Mali. Vikosi vya wanajeshi 2,400 wa Ufaransa vimekuwepo nchini Mali kwa takriban miaka 10 kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi.
Mvutano kati ya Ufaransa na Mali ulipamba moto katika miezi ya hivi karibu baada ya mapinduzi ya kijeshi ya 2021 katika nchi hiyo ya Magharibi mwa Afrika, wakati Kanali Assimi Goïta alipotwaa madaraka ya nchi.
Maafisa wa serikali ya Mali wanawatuhumu wanajeshi wa Ufaransa kuwa wanashirikiana na makundi ya kigaidi yanayotaka kujitenga eneo la kaskazini mwa nchi hiyo, kufanya ukatili dhidi ya raia na kushindwa kukabiliana ipasavyo na makundi ya kigaidi.
Baada ya Baraza la Kijeshi la Mali kuanza kazi lilitangaza kuwa haliyatambui makubaliano ya ulinzi baina ya nchi hiyo na Ufaransa na kwamba halitayatekeleza. Serikali ya Mali pia ilimfukuza balozi wa Ufaransa mjini Bamako, kitendo ambacho kilikabiliwa na hisia kali ya serikali ya Paris.