Wanajeshi watatu wa utawala wa Kizayuni wamejeruhiwa katika operesheni ya kukimbizana na magari katika eneo la Negebu
Vyanzo vya utawala wa Kizayuni vimeripoti kuwa, askari watatu wa utawala huo wamejeruhiwa katika operesheni ya kuwakimbiza magari katika eneo la Negev, lililoko kusini mwa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.
Wakati huo huo, vyombo vya habari vya Kiebrania viliripoti Jumapili iliyopita jioni kwamba vikosi vya muqawama wa Palestina vililishambulia kwa risasi basi lililokuwa limebeba Wazayuni karibu na makazi ya Wazayuni ya “Mafo Dotan” karibu na Jenin iliyoko katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kanali ya 14 ya Televisheni ya utawala wa Kizayuni ilitangaza kuwa basi lililokuwa limebeba walowezi lilipigwa risasi karibu na makazi hayo ya Wazayuni karibu na Jenin, kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Duru za Kiebrania zilisema kuwa mjumbe wa Knesset ya utawala wa Kizayuni alikuwa miongoni mwa Wazayuni kwenye basi hili.
Yossi Yehoshua, ripota wa kijeshi wa gazeti la Yediot Aharonot aliwahi kukiri hapo awali kwamba, serikali mpya ya utawala wa Kizayuni haitaweza kusimamisha operesheni za muqawama wa Palestina dhidi ya askari na walowezi wa Israel katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.