Harakati ya Muqawama ya Asa’ib Ahl al-Haq ya Iraq imelitaka Bunge la nchi hiyo lichukue hatua za kivitendo kujibu mashambulizi ya anga ya Uturuki katika eneo la Kurdistan, lililoua na kujeruhi makumi ya raia.
Katika taarifa, kundi hilo la muqawama nchini Iraq limeihutubu Uturuki kwa kusema: Uvamizi, kuendelea kukiuka mamlaka ya kujitawala Iraq, kukalia kwa mabavu baadhi ya maeneo ya nchi hii, kuanzisha kambi za kijeshi, na kumwaga damu za raia, yote hayo yapo mbali na misingi ya ujirani mwema na hati za kimataifa.
Harakati ya Muqawama ya Asa’ib Ahl al-Haq ya Iraq imetoa mwito wa kuungana serikali, Bunge na mirengo ya kisiasa ya nchi hiyo ya Kiarabu, kwa shabaha ya kupambana kwa pamoja na chokochoko za wavamizi.
Jeshi la Uturuki lilifanya shambulio katika kituo cha utalii katika mkoa wa Zakho ulioko katika eneo la Kurdistan ya Iraq Jumatano, na kuwauwa wanawake na watoto wasiopungua 11.
Serikali ya Ankara imedai kuwa, uwepo wa kundi la Kikurdi la PKK ndio sababu ya kuyashambulia maeneo ya kaskazini mwa Iraqi.
Harakati ya Asa’ib Ahl al-Haq ya Iraq imelitaka Bunge la nchi hiyo liandae mazingira ya kufukuzwa wanajeshi wa Uturuki, na kuhitimisha uwepo wa askari ajinabi nchini humo kwa kufunga kambi zao zote