Matokeo ya uchunguzi mpya wa maoni uliofanywa hivi karibuni huko Marekani yanaonyesha kuwa akthari ya wapiga kura wa nchi hiyo wanapinga Joe Biden na Donald Trump, rais wa sasa na wa kabla yake, kugombea tena katika uchaguzi wa rais mwaka 2024.
Uchaguzi ujao wa rais wa Marekani umepangwa kufanyika tarehe 5 Novemba mwaka 2024.
Shirika la habari la Iran, IRNA, limeripoti kuwa, uchunguzi mpya wa maoni uliofanywa na Taasisi ya Rasmussen unaonyesha kuwa asilimia 55 ya wananchi wa Marekani wanasema Rais wa sasa wa nchi hiyo, Joe Biden hapasi kugombea tena muhula mwingine wa urais.
Wakati huo huo asilimia 33 ya watu walioshiriki katika utafiti huo wa maoni uliosimamiwa na Taasisi ya Rasmussen wanaafiki Biden kugombea tena kiti cha urais mwaka 2024, na asilimia 11 wamesema kuwa bado hawajachukua uamuzi katika uwanja huo. Uchunguzi huo mpya wa maoni umeweka wazi kuwa, asilimia 78 ya Warepublican na asilimia 62 ya wasio na vyama wanasema kuwa Biden hapasi kushiriki tena katika uchaguzi wa rais wa mwaka 2024.
Uchunguzi huo mpya wa maoni umeongeza kuwa, asilimia 53 ya wapiga kura Marekani wanapinga Donald Trump kugombea tena kiti cha rais mwaka 2024. Wakati huo huo asilimia 35 ya wapiga kura wamesema kuwa wanaafiki rais huyo wa zamani wa Marekani agombee tena kiti cha urais, na asilimia 11 hawajaamua iwapo Trump ashiriki uchaguzi wa mwaka ujao au la.
Akiwa mbele ya wafuasi wake, Trump mara kadhaa amewatuhumu Wademocrat kuwa walifanya udanganyifu mkubwa katika uchaguzi wa rais uliopita kwa maslahi ya Rais wa sasa wa Marekani, Joe Biden.