Wananchi wa Burkina Faso washerehekea kuondoka kwa wanajeshi wa Ufaransa nchini humo

Wananchi wa Burkina Faso wamepokea kwa furaha na shangwe taarifa ya kufikia tamati uwepo wa wanajeshi wa Ufaransa katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Wananchi wa Burkina Faso wameziambia duru mbalimbali za habari kwamba, wana furaha kubwa baada ya wanajeshi wa Ufaransa kuondoka katika nchi yao.

Baadhi ya wananchi hao wamesema, kuondoka wanajeshi hao kilikuwa kilio cha muda mrefu cha wananchi na serikali ya Burkina Faso.

Ufaransa na Burkina Faso zilisimamisha rasmi operesheni za jeshi la Ufaransa katika taifa hilo la Afrika Magharibi.

Taarifa ya jeshi la Burkina Faso imeeleza kuwa, jana Jumapili ilikuwa siku ya mwisho ya ushirikiano wa kijeshi baina ya mataifa hayo mawili. Taarifa hiyo ilitolewa baada ya kufanyika hafla ya kushusha bendera ya vikosi vya Ufaransa ambayo iliashiria kufikia tamati uwepo wa vikosi vya Ufaransa katika nchi hiyo ya Kiafrika.

Mwezi uliopita wa Januari, Burkina Faso iliipa Ufaransa mwezi mmoja iwe imeondoa vikosi vyake wakati ikimaliza makubaliano ya kijeshi, yaliyoruhusu vikosi vya Ufaransa kupambana na waasi katika himaya yake, ikielezea kuwa nchi itajilinda yenyewe.

Uamuzi wa Burkina Faso wa kuwatimua wanajeshi wa Ufaransa ni ushahidi wa kuzidi kuzorota uhusiano kati ya Ufaransa na koloni lake la zamani baada ya mapinduzi ya kijeshi ya mwezi Septemba 2022.

Baadhi ya mivutano hiyo inatokana na ukweli kwamba uwepo wa jeshi la Ufaransa nchini Burkina Faso haujaimarisha usalama katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika na wananchi wa Burkina Faso wanaamini kwamba, ni wakoloni hao wa Ulaya ndio wanaochochea machafuko, mapinduzi ya mfululizo ya kijeshi, vitendo vya kigaidi na ukosefu wa usalama nchini humo.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *