Wanazuoni wa Bahrain wanaosota kwenye jela za utawala wa kifalme wa nchi hiyo wa ukoo wa Aal Khhalifa wameeleza katika taarifa waliyotoa kumhutubu Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis kwamba, wanatumai kiongozi huyo wa kidini atasema ukweli na kuitikia wito wa imani katika ziara yake ijayo huko Bahrain.
Shirika la habari la IRNA limeripoti leo kuwa, wanazuoni wa Bahrain wanaoshikiliwa katika jela za utawala wa kiimla wa Aal Khalifa wameeleza katika taarifa yao wakimhutubu Papa Francis, ambaye atakuweko Bahrain kuanzia tarehe 3 hadi 6 Novemba kushiriki mkutano wa “Mazungumzo baina ya Mashariki na Magharibi”: “wewe utaweka mguu wako katika ardhi ya nchi ambayo kauli mbiu ya kuvumiliana na kuishi pamoja inatolewa kwa ajili ya wananchi; na kubainishwa ndani yake haki, uadilifu na ihsani; lakini dhulma na utovu wa haki vimeenea ndani yake”.
Taarifa hiyo imetolewa kwa jina la Sheikh Abdul Jalil al-Miqdad, Sheikh Saeed al-Nuri, Sheikh Muhammad Habib al-Miqdad na Sheikh Ali Salman, ambao ni maulamaa wa Bahrain waliokamatwa na kufungwa jela na utawala wa Aal Khalifa kwa sababu za kisiasa.
Sehemu nyingine ya taarifa ya wafungwa hao wanne wanaosota katika jela za utawala wa kifalme wa Bahrain inasema: “watu wa ardhi hii ni miongoni mwa waliofariki, akina mama wenye majonzi makubwa ya kuondokewa, watu waliojeruhiwa, wafungwa, wanaosakwa na waliohamishwa kwa kupelekwa mbali na nchi yao na familia zao zilizobaki katika ardhi yao katika hali ya kusubiri.
Mwishoni mwa taarifa yao, wanazuoni hao wanne wa Bahrain wamesema wana matumaini kuwa Papa Francis atazungumza ukweli wakati wa ziara yake nchini Bahrain na “kuitikia wito wa imani na akili iliyo timamu.”
Tangu Februari 14, 2011 Bahrain imekuwa uwanja wa mapambano ya amani ya wananchi dhidi ya utawala wa kiimla wa ukoo wa Aal Khalifa. Wananchi hao wanataka uhuru, kutekelezwe uadilifu na kuondolewa ubaguzi pamoja na kuongozwa na serikali waliyoichagua wenyewe.