Jumuiya ya Ulaya ya kutetea na kuunga mkono Quds tukufu (Jerusalem) imetangaza kuwa katika kipindi cha mwezi mmoja, askari wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel wamevamia mji huo wa Baitul Muqaddas unaokaliwa kwa mabavu na kuwatia nguvuni Wapalestina zaidi ya 190 wakazi wa mji huo.
Hujuma na mashambulio ya askari wa utawala wa Kizayuni dhidi ya Quds inayokaliwa kwa mabavu na Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan na mapigano kati yao na Wapalestina yameongezeka katika miezi ya hivi karibuni.
Jumuiya ya Waulaya waungaji mkono wa Quds imeeleza katika ripoti kuwa, katika mwezi uliopita wa Februari, Wapalestina 191, wakiwemo watoto 16 na wanawake 16 walitiwa mbaroni na askari wa utawala haramu wa Israel.
Kituo cha upashaji habari cha Palestina nacho pia kimetangaza kuhusiana na suala hilo kuwa, Wapalestina 221 wakiwemo makumi ya wanawake na watoto wamejeruhiwa katika mapigano yaliyotokea mwezi uliopita mjini Baitul Muqaddas inayokaliwa kwa mabavu.
Kwa mujibu wa kituo hicho, ndani ya kipindi hicho cha mwezi Februari, utawala wa Kizayuni umebomoa pia nyumba 14 za Wapalestina katika mji huo na kuziacha familia za Wapalestina 82 zikibaki bila makazi.
Utawala dhalimu wa Kizayuni wa Israel umepanua wigo wa operesheni ya kuwatia nguvuni Wapalestina hususan vijana katika eneo la Ufukwe wa Magharibi ili kuzima wimbi la harakati za kupambana na utawala huo ghasibu.
Takwimu zinaonyesha kuwa, kamatakamata hiyo na kuwaweka kizuizini Wapalestina, si tu haijaweza kupunguza nguvu ya operesheni za muqawama, lakini katika mwaka uliopita, opereseni hizo dhidi ya uzayuni zimeongezeka kwa kiwango kikubwa…/