FARAAN: Hayo yameripotiwa na shirika la habari la Wafa ambalo limeeleza kuwa, vijana hao wa Kipalestina wameuawa shahidi alfajiri ya leo Ijumaa baada ya wanajeshi makatili wa Israel kushambulia kambi ya wakimbizi huko Jenin.
Habari zaidi zinasema kuwa, Wapalestina hao wameuawa shahidi baada ya gari lililokuwa limewabeba kumiminiwa risasi na wanajeshi hao wa Israel, ambao pia wamejeruhi Wapalestina wengine 10.
Duru za hospitali katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu zimewataja wahanga hao waliouawa kikatili kwa risasi za Wazayuni kuwa Youssef Nasser Salah, 23, Baraa Kamal Lahlouh, 24, na Laith Salah Abu Srour, 24.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Palestina, Wapalestina zaidi ya 70 wameuawa shahidi na wanajeshi makatili wa utawala wa Kizayuni wa Israel tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2022 hadi sasa.
Jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel katika miezi ya hivi karibuni limelazimika kusitisha mara kadhaa mashambulizi yake dhidi ya mji wa Jenin, likihofia majibu ya makundi ya wanamapambano wa Kipalestina. Vikosi vya muqawama vya Palestina vimeonya kuwa, hatua yoyote ya kijeshi ya utawala haramu wa Israel katika mji wa Jenin, haitapita hivi hivi bila kupatiwa jibu kali.