Makumi ya maelfu ya Waislamu wa Palestina jana walishiriki katika ibada ya Sala ya Ijumaa kwenye Kibla cha Kwanza cha Waislamu yaani Msikiti wa al Aqsa, licha ya vikwazo vingi vya utawala wa Kizayuni.
Hayo yameripotiwa na Shirika la Habari la Tasnim ambalo limezinukuu duru za Palestina zikitangaza kuwa, Sala ya Ijumaa ya jana katika Msikiti wa al Aqsa mesaliwa na makumi ya maelfu ya waumini.
Duru hizo zimeeleza kuwa, Wapalestina 75,000 walishiriki katika Sala ya Ijumaa hiyo jana licha ya kuwekewa vikwazo vikubwa vya jeshi la utawala wa Kizayuni katika milango ya kuingilia Msikiti wa al Aqsa.
Jumuiya ya Wakfu ya Beit Al-Maqdis imetangaza kuwa, Wapalestina 75,000 wanaoishi katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, Baitul Muqaddas na maeneo 48 yanayokaliwa kwa mabavu na Wazayuni walifika katika Msikiti wa al Aqsa baada ya kuvuka vizuizi vikali vilivyowekwa na jeshi la utawala wa Kizayuni na wamefanikiwa kusali Sala ya Ijumaa katika eneo hilo takatifu kiukamilifu na kwa hamasa kubwa.
Wavamizi Wazayuni waliweka vizuizi kwenye maeneo mengi ya Baytul Muqaddas na walisimamisha kila gari ya Mpalestina kwenye milango ya kuingilia eneo la Msikiti wa al Aqsa na kukakagua hati za vitambulisho za Wapalestina.
Sheikh Youssef Abu Sunina, anayetoa khutba kwenye Msikiti mtakatifu wa al Aqsa alisema katika khutba za Sala ya Ijumaa ya jana kwamba Msikiti wa al Aqsa ni muhanga wa uvamizi wa kikatili wa utawala wa Kizayuni.
Ameashiria pia kwamba Waislamu watakilinda Kibla chao cha Kwanza wakiwa ni ngome imara na amesema kuwa, kuna wajibu wa kudhaminiwa haki za wafungwa wa Kipalestina na kukabidhiwa miili ya mashahidi wa Kipalestina kwa familia zao.